Taasisi ya Al-Azhar Observer ya Chuo Kikuu cha al Azhar cha imesema katika ripoti yake kuwa, matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu katika vyombo vya habari vya Magharibi yameongezeka huku mitandao ya kijamii ikitumika kuchochea waziwazi chuki hizo bila ya udhibiti wowote.

Kwa mujibu wa Al-Bawaba News, Al-Azhar Observer imesema katika ripoti yake hiyo kwamba: Chuki dhidi ya Waislamu zimeonekana katika matukio mengi, na moja ya kesi za kusikitisha zaidi za zama hizi ni mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar ambayo kampeni nyingi za chuki na upotoshaji ulienezwa kupitia mitandao ya kijamii dhidi ya Waislamu wa jamii hiyo.

Ripoti hiyo inaongeza: Wanasiasa wengi wa Ulaya wenye chuki na Uislamu wana mchango mkubwa katika kuongezeka chuki hizo kwa sababu wafuasi wa wanasiasa hao hasa vijana wa Ulaya, wanaathiriwa na mazungumzo ya ubaguzi wa rangi dhidi ya wageni kwa ujumla na hasa Waislamu. Kumeripotiwa kesi nyingi za hata kuuliwa kwa umati Waislamu kutokana na maneno ya chuki yanayoenezwa na wanasiasa maadui wa Uislamu katika nchi za Magharibi.

Al-Azhar Observer imeongeza kuwa, kushamiri chuki hiyo na kuenea mno katika jamii, kumeziweka kwenye wakati mgumu na kuzitumbukiza kwenye hatari kubwa juhudi za kuhakikisha watu wanaishi pamoja na amani. Tafiti nyingi za hivi karibuni zinaonesha kwamba vyombo vya habari vya Magharibi vimepotosha zaidi ukweli kuhusu Uislamu na kuchochea mauaji na vitendo vya kikatili dhidi yao kuliko watu wa jamii nyinginezo zote. Matokeo ya tafiti hizo yanaonesha pia kuwa, vyombo hivyo vya habari vinachochea mno hisia za uadui dhidi ya Waislamu; kitendo ambacho kinaathiri vibaya hali za Waislamu katika nchi za Magharibi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Azhar Observer, watafiti wawili wa Sayansi ya Jamii ambao hata si Waislamu, (Eric Bleich na Moritz van der Veen) wamefanya utafiti wa kina unaoonesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Waislamu.

Watafiti hao wanasisitiza katika utafiti wao kwamba baada ya kuchambua zaidi ya nakala laki 7 na 84,000 za magazeti katika kipindi cha miaka 20, zikiwemo nakala laki mbili na 56,000 kutoka Marekani na nakala laki na 28,000 kutoka Uingereza, Canada na Australia katika kipindi cha baina ya 1996 na 2016, walifikia hitimisho kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Waislamu na kwamba Waislamu wamekumbwa na mitazamo mingi zaidi hasi ikilinganishwa na wafuasi wa dini nyingine.

Uchanganuaji wa data hizo unaonesha kuwa wastani wa idadi ya makala nchini Marekani zinazohusu Waislamu au Uislamu ni takriban asilimia 84, wakati makala zinazohusu Wakatoliki, Mayahudi, Wahindu au kikundi kingine chochote ni chache mno. Kati ya makundi hayo, kumekuwa na wastani sawa wa asilimia 50 kwa 50 wa maelezo chanya na hasi katika nakala hizo kuhusu makundi yasiyo ya Kiislamu wakati maelezo ya chuki na hasi dhidi ya Waislamu katika vyombo hivyo ni asilimia 80 ikilinganishwa na maelezo chanya juu yao.

(Visited 18 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!