Mamlaka za Oman zimetangaza kuwa, kuanzia kesho Jumanne, Disemba 22, 2020, nchi hiyo itafunga mipaka yake yote ya ardhini, angani na baharini kwa muda wa wiki moja katika hatua za tahadhari za kujiepusha na maambukizi ya spishi mpya ya kirusi cha corona iliyoshuhudiwa nchini Uingereza. Zoezi hilo litaanza saa saba mchana kesho Jumanne kwa saa za Oman.

Shirika la habari la Mehr limeunukuu mtandao wa al Nashra ukitangaza habari hiyo na kuthibitisha kwamba mipaka yote ya ardhini, angani na baharini itafungwa nchini Oman kuanzia Jumanne, Disemba 22, 2020 kwa muda wa wiki moja.

Hatua hiyo ya Oman imekuja baada Kuwait nayo kutangaza hatua hiyo hiyo kuanzia leo Jumatatu hadi Januari 1, 2021. Kuwait imetangaza kuwa, safari zote za ndege za biashara za kutoka na kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuwait City zimesimamishwa na mipaka yote ya ardhini na baharini imefungwa kuanzia leo saa 5 usiku kwa majira ya nchi hiyo hadi Januari 1, 2021.

Taarifa nyingine zinasema kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, ameitisha kikao cha dharura cha kujadili wimbi la maambukizi ya kirusi kipya cha corona kilichogunduliwa kusini mwa nchi hiyo.

Nchi nyingi za Ulaya zimekata mawasiliano yao na Uingereza huku Saudi Arabia nayo ikitangaza wiki moja ya marufuku ya safari za ndege zote za kimataifa, kuingia na kutoka nchini humo.

Katika upande mwingine, Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa inafanya mazungumzo na Russia na China kuhusu kununua chanjo za COVID-19 zilizotengenezwa na nchi hizo. Tayari shehena tatu za chanjo ya corona iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya Ujerumani na Marekani, zimeshawasili nchini Saudi Arabia. Mamlaka husika za nchi hiyo zimetangaza kwamba, nia yao ni kuwapiga chanjo ya corona wananchi wote wa Saudia.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!