Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?

? QURAN TUKUFU ?

Aya ya Leo…

? Al-Kahfi 18:09 ?

(أَمۡ حَسِبۡتَ أَنَّ أَصۡحَـٰبَ ٱلۡكَهۡفِ وَٱلرَّقِیمِ كَانُوا۟ مِنۡ ءَایَـٰتِنَا عَجَبًا)

Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?

??????????

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Hapa ndipo kinapoanza kusimuliwa kisa maarufu cha Watu wa Pango.

Huko nyuma tulisema kwamba visa vya Qur’ani vikiwemo hivi vitano vya sura ya 18 ya al Kahf vina mafundisho mengi sana.

Lakini kwa nini neno al Raqim hapa. Nini asili ya neno al Raqim? Je, ni kundi moja la watu au ni makundi mawili, yaani Aswhabul Kahf ni mbali na Aswahab al Raqim ni mbali? Wanachuoni wametoa kauli tofauti. Lakini si makusudio yangu hapa kunukuu hayo. Lengo langu leo ni kitu kingine.

Kisa cha Aswhabul Kahf kimesimuliwa kwenye aya 18 zilizofuatana ndani ya sura ya 18 ya Al Kahf.

Tuzigawe aya hizo mafungu mawili makuu. Fungu la kwanza ni la aya 4 za mwanzo na fungu jingine ni la aya 14 za pili.

Natamani ufungue Mas’haf uziangalie hizo aya na mafungu yake mawili. Aya 4 za kwanza na baadaye aya 14 za pili utagundua kuwa, kisa chote kimo kwenye aya 14 za pili. Aya 4 za mwanzo ni muhtasari wa kisa kizima. Naam, aya nne za mwanzo ni dondoo muhimu za kisa chenyewe.

Mbinu hii ya kusimulia kisa ni ya balagha ya hali ya juu sana. Ni mbinu ambayo waandishi wote leo hii wameiiga. Hii ni mbinu ya kuanza na utangulizi wenye dondoo muhimu na muhtasari wa matni yote inayofuata.

Hebu angalia waandishi wakuu wa vitabu, hukupa muhtasari kwanza, imma upande wa nyuma wa jalada au ndani ya kitabu.

Angalia magazeti, lazima kurasa za mbele zinakuwa na dondoo na muhtasari wa habari kamili za kurasa za ndani.

Angalia tovuti na website zote muhimu na zenye itibari, lazima utapata muhtasari na utangulizi wa habari husika ambapo umbuji wa mwandishi huonekana pale anapohakikisha muhtasari wake unabeba sehemu muhimu zaidi ya alichokiandika na kumkinaisha mtu kununua na kusoma alichoandika.

Ukiangalia aya 4 za kwanza za kisa cha Aswhabul Kahf utaona zinakupa dondoo na muhtasari wa kisa kizima kwa njia bora kabisa.

Kisa kimeanza na mbinu ya Amhasibta. Nakumbuka tulisema mengi kuhusu mbinu hiyo wakati tulipozungumzia Alamtara katika kisa cha Nabii Shamueli, Nabii Daud na Talut na Jalut. Mbinu hiyo ndiyo ambayo hapa pia Allah ameitumia kusimulia kisa cha Watu wa Pango.

Tulisema juzi kwamba kama utazingatia visa vya Surat al Kahf na mbinu zake, unaweza kuanzisha somo maalumu vyuo vikuu tena si kwa Waislamu tu. Kila mwandishi anahitajia mno kuzitambua kwa kina mbinu za Qur’ani Tukufu zikiwemo hizi za Alamtara, Amhasibta na za kutoa dondoo muhimu na muhtasari wa alichokusudia kukiandika.

Angalia matangazo ya redioni na kwenye televisheni. Lazima utaona wana muhtasari na vichwa vya habari muhimu na huu muhtasari na vichwa vya habari muhimu ndio unaobakia sana kwa walengwa. Hayo yamethibitishwa na uchunguzi wa kivitendo wa wasomi na wataalamu wakubwa wa saikolojia.

Mbinu hiyo inatumiwa pia na mabingwa wa kuandika CV na Resume za watu kwa ajili ya mashirika makubwa ya ajira na wanakwambia kuwa watu hawana muda, sema lililo muhimu zaidi kwa muhtasari watu wakuelewe. Mbinu hii ya kuandika CV na Resume ina wataalamu wake wanaouza ujuzi wao kuwafanyia wengine.

Hii mbinu inatumiwa pia na watu wa filamu na sinema. Kuna kitu kinaitwa Trailer ambacho kinatengenezwa kutoa muhtasari na dondoo za filamu nzima kwa sura ya kuvutia kabisa mpaka watu wanapanga foleni kwenda kuzitazama filamu hizo.

Yote haya ya uandishi wa riwaya, habari, vitabu n.k kwa namna hii ya leo, umekuja baadaye sana baada ya kutumiwa miaka mingi nyuma na Qur’ani Tukufu.

Waacheni Waislamu wawe wakali mno kila anapotokea fidhuli kukifanyia ufidhuli Kitabu chao kitakatifu.

Mwanafunzi wenu, Ahmed Rashid.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

(Visited 24 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!