Chama cha maquraa na wasomaji wa Qur’ani Tukufu nchini Misri kimeweka sheria mpya za kudhibiti washingiriaji wakati maqari wanaposoma Qur’ani katika majlisi za misiba.

Mtandao wa habari wa “al Akhbar al Yaum” wa nchini Misri umeripoti habari hiyo na kumnukuu Sheikh Muhammad Saleh Hashad, mkuu wa chama cha maquraa wa Misri akisema kuwa, baraza kuu la chama hicho limekutana na kuamua kwamba, kumekuwa na mtindo wa baadhi ya watu kutoheshimu vikao vya maombolezo na majonzi wakati wasomaji wa tajwidi wanaposoma Qur’ani kwenye majlisi hizo, hivyo kuna wajibu wa kudhibitiwa watu hao.

Amesema, haifai watu waruhusiwe kushangiria kupita kiasi na kwa sauti za fujo wakati Qur’ani inaposomwa hasa kwenye majlisi za watu wenye huzuni hivyo maqari nao wanatakiwa wadhibiti hadhirina wakati wanaposoma tajwidi.

Sheikh Shahad amesema, qari yeyote atakayekwenda kinyume na sheria hizo mpya atapelekwa mbele ya vitengo husika.

Ameongeza kuwa, mtu yeyote anayekuwa mwanachama cha chama cha maquraa cha Misri, lazima awe amehifadhi Qur’ani nzima na vikao vikuu vya chama ndivyo vinavyoamua nani awe mwanachama. Sheria hizo mpya zimechukuliwa baada ya baadhi ya maquraa na wasomaji tajwidi kuonekana wanajali tu umaarufu na malipo na hiyo ni bidaa hatari sana inayokwenda kinyume na mafundisho ya Qur’ani Tukufu.

(Visited 1 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!