Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh, ndugu zangu wapendwa. Kusema kweli hakuna mafundisho yoyote sahihi ya Uislamu yaliyowekwa juzafa, bure bilashi bila ya kuwa na hekima maalumu. 

Naam, kila nukta ya mafundisho hayo matukufu ya Uislamu yamejaa hekima na manufaa makubwa ya kiroho, kimwili, kijamii na kila kitu. Hakuna chochote kilichoamrishwa na Uislamu ila kina manufaa na hakuna chochote kilichokatazwa na dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu ila kina madhara. Maamrisho yote ya Uislamu yako makini mno katika kubainishwa kwake. Ile herufi moja tu katika mafundisho ya Uislamu basi ina maana pana katika kutangulia kwake kuja, katika kutumika kwake, na katika kila kitu. Kwa mfano katika kalimatutawhid ambayo ndio ufunguo wa mtu kuwa Muislamu, neno lililotangulia kabla ya jambo lolote ni “laa” Yaani Laailaaha Illa Llah Muhammadurrasullullah. Yaani neno hilo tukukfu mno limeanza kwa kukanusha, hakuna mungu, sasa lazima mtu atajiuliza na atadadisi kwa mshangao na atasema: Hakuna mungu? Inawezekana kweli hakuna mungu? Hapo hapo majibu yakaja kwa istithnaa, illallah! Isipokuwa Mungu Mmoja tu, Allah! Subhanallah! Wanachuoni wamechambua vyema kwa nini likatangulia neno laa katika kalimatutawhid. Mfano mwingine kwa haraka haraka, ni wa jinsi Mwenyezi Mungu alivyolitanguliza na kuliakhirisha neno khalifa katika aya za 30 ya Sura ya pili ya al Baqarah na aya ya 26 ya 38 ya Swad. Katika sehemu moja ya aya ya 30 ya al Baqarah tunasoma: 

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الأَرْضِ خَلِيفَةً

Na pale Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa

Na katika Surat al Swad sehemu moja ya aya ya 26 tunasoma

يَادَاوُودُ إِنَّا جَعَلْنَاكَ خَلِيفَةً فِي الأَرْضِ

Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika ardhi.

Katika aya hizo mbili kuna mfanano mwingi, inna ya msisitizo imetumika kote kuwili, neno ja’ala pia limetumika kote kuwili, herufi fii na maneno ardh na khalifa yote yametumika kwenye aya zote mbili. Lakini pia kuna tofauti kubwa baina ya aya hizo mbili. Neno ardhi limelitangulia neno khalifa katika aya ya 30 ya Surat al Baqarah wakati katika aya ya 26 ya Surat al Swad, neno khalifa limelitangulia neno ardhi! Hekima yake ni nini? Mabingwa wa tafsiri wamelichambua hilo. Na mifano hiyo imejaa tele ndani ya Qur’ani Tukufu na si lengo langu leo kuzungumzia jambo hilo. Ninachotaka kutilia mkazo tu hapa ni kwamba, kuna hekima kubwa katika kila neno, kila herufi na kila kutangulizwa na kuakhirishwa neno fulani ndani ya aya za Qur’ani na hadithi sahihi. Naam, kuna maana na hekima zake kubwa. Amma nilichokusudia kusema hapa leo ni hii hekima ya kufunga siku tatu mfulilizo katika mafundisho ya Uislamu yaliyomo kwenye Qur’ani Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume Muhammad SAW.

Mbali na Qur’an kusema wazi kwamba kufunga saumu ni bora kwetu, imehimiza pia kwa mfano watu wanaokula yamini na kiapo cha uongo wafunge siku tatu mfululizo, au wanaoshindwa kuwa na mnyama wa kuchinja wafunge siku tatu katika Hija na saba wakirejea. Au himizo la Bwana Mtume la kusisitiza kwamba fungeni ili mpate siha, au hatua yake ya kuziita funga za Ayyam al Biidh, siku nyeupe kila mwezi kuwa ni sawa na kufunga dahari nzima. Kuna siri gani katika funga ya siku hizi tatu za mfululizo ambazo zimetiliwa mkazo sana na Uislamu? Manufaa ya kiroho, kijamii na kiafya na ya kila kitu ni makubwa sana katika mafundisho hayo na sisi Waislamu tunaona fakhari kuwa na mafundisho matukufu kama haya. Lakini inapotokezea wasio Waislamu kufanya uchunguzi wao huru na kugundua ubora wa mafundisho ya Uislamu, imani yetu bila ya shaka yoyote inazidi kuwa kubwa. Hivyo nilichokusudia leo ni kunukuu utafiti wa kiutaalamu uliofanywa na Dk Abduldaem al Kaheel wa nchini Syria ambaye amelifanyia utafiti suala hilo na kusema: Chuo Kikuu cha Kusini mwa California nchini Marekani kimefanya utafiti usio wa kawaida wa kutafuta njia bora kabisa ya kuongeza na kufufua nguvu za mwili wa mwanadamu za kujikinga na maradhi na kuzifanya nguvu hizo kuwa imara zaidi na matokeo ya utafiti huo yalikuwa ya kustaajabisha mno. Naam, uchunguzi huo umeonesha kwamba njia bora kabisa ya kufufua nguvu za mwili za kujikinga na maradhi ni kufunga siku tatu mfululizo. Uchunguzi huo uliendelea kwa muda wa miezi sita huko California Marekani na ulishirikisha watu wa aina mbalimbali. Mwishowe wanasayansi waligundua kwamba, mwili wa aliyefunga siku hizo tatu ulifanikiwa kusafisha sumu zilizokuwa zimerundikana mwilini pamoja na seli mbovu ambazo zilikuwa ni sawa na uchafu mwilini. Aidha nguvu za mwili za kujikinga na maradhi zilikuwa kubwa zaidi katika kupambana na virusi baada ya kufunga siku tatu mfululizo.

Dk Abduldaem anaendelea kusema: Profesa Valter Longo anasema kwa kujiamini kwamba, katika kipindi cha siku tatu cha funga ya mfululizo, na wakati mwili wako unapoona njaa, huwa unapata nafasi ya kujisafisha na seli chafu zilizokufa na zilizoharibika ambazo hazitakiwi mwilini na baada ya hapo mwili huanza kuzalisha seli nyeupe za damu ambazo zina nguvu kubwa zaidi, amilifu zaidi na zenye athari bora zaidi katika kupambana na virusi. Wakati mwili wa mwanadamu unapoanza kufunga saumu, hupungua ghafla seli nyeupe na mara mtu unapoingiza chakula kingine mwilini, huanza kuzalisha upya seli hizo nyeupe za kupambana na virusi. Profesa Longo anasema kwa kujiamini kabisa kwamba, wakati seli zako mwilini zinapokufanya uhisi njaa, seli hizo hupata nguvu kubwa zaidi za kuhimili matatizo na kuishi kwa muda mrefu. Na anasema pia kwa kujiamini kwamba, mtu anapofunga kwa muda wa siku tatu, mwili wake hutoa idhini ya kujengeka upya seli kuu ambazo ni muhimu zaidi mwilini kiasi kwamba huunda mfumo mpya wa kujikinga na maradhi katika funga ya siku tatu tu. Katika kipindi cha siku hizo tatu za funga, mwili hujisafisha na baadhi ya seli zilizokuwemo kwenye mfumo wa huko nyuma wa mwili wa kuhimili maradhi na huziondoa kabisa seli ambazo tayari zilikuwa zimeshachoka na zimeshaharibika na hujenga mfumo mwingine mpya wa kujikinga na maradhi ambao ni imara na madhubuti zaidi ambao una nguvu za kugundua kwa njia bora virusi na kukabiliana navyo kwa namna bora kabisa. Sasa hapa linazuka swali, njia gani bora zaidi ya kufunga siku hizo tatu mfululizo? Swali hilo limejibiwa na wasomi na wataalamu wa zama hizi. Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanyika Chicago Marekani ambao matokeo ya uchunguzi huo yamechapishwa kwenye jarida la Nutrition and Healthy Aging unaonesha kuwa, njia bora kabisa ya kupata athari nzuri za funga hiyo ya siku tatu ni ile inayoitwa 16-8. Njia hiyo ina taathira kubwa katika kuuwezesha mwili wa mwandamu kupata faida tulizotangulia kusema za funga ya siku tatu mfululizo na ambayo pia ndiyo njia nyepesi na rahisi zaidi mtu kwenda nayo. Labda ndugu yangu utajiuliza, hiyo mbinu ya 16-8 ni kitu gani? Njia hiyo maana yake ni kwamba mtu afunge muda wa masaa 16 bila ya kula chochote na ale na anywe katika kipindi cha masaa manane yaliyiobakia kila siku katika siku hizo tatu mfululizo. Sasa ukiangalia utaona kuwa mbinu hiyo iliyotajwa na wasomi wa nchi za Magharibi, inafanana mno na namna Waislamu wanavyotekeleza ibada ya funga. Lakini je, Bwana Mtume Muhammad SAW, aliyewatangulia wasomi na wataalamu wote, alilinyamazia kimya jambo hili? Je, hakutufundisha chochote kuhusu uhakika huu wa kimatibabu wenye faida kubwa kwa mwili wa mwanadamu? Hapana, hakulinyamazia jambo hilo. Bwana wetu na kipenzi chetu, Muhammad al Mustafa SAW ametuhimiza tuwe tunafunga mara kwa mara kila mwezi zikiwemo siku tatu mfululizo zinazojulikana kwa jina la Ayyam al Biidh. Ametuhimiza sana jambo hilo mpaka ametueleza kwamba mwenye kufunga siku hizo ni kama aliyefunga dahari nzima neno ambalo baadhi wanalifasiri kwa maana ya mwaka na wengine kwa maana ya zama n.k. Bwana Mtume amenukuliwa akisema, Swiyamu thalathati Ayyamin min kulli shahr, swiyamud Dahr.

Funga ya siku tatu za kila mwezi ni funga ya dahari. Siku hizo tatu ambazo kama tulivyosema ni maarufu kwa jina la Ayyamil Biidh, siku tatu nyeupe, ni zile siku za mwezi mdande, yaani wakati mwezi unapokuwa umekamilika na ukawa unang’ara kabisa nazo ni mwezi 13, 14 na 15 yaani tarehe 13 na kumi na nne na kumi na tano za kila mwezi mwandamo, wa kalenda ya Kiislamu inayofuata mwandamo wa mwezi si mwezi wa jua. Hadithi hiyo inapatikana kwenye vitabu vikubwa na maarufu vya hadithi. Hii ni kana kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW anataka kutwambia kuwa, ufanyeni wa kisasa mfumo wa miili yenu wa kujikinga na maradhi kila mwezi ili miili yenu ibakie na siha, imara, salama na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na maradhi na virusi mbalimbali. Swali la mwisho linalojitokeza hapa ndugu zangu wapendwa ni kwamba, vipi Bwana Mtume Muhammad SAW alijua mambo yote haya, zaidi ya karne kumi na nne zilizopita? Vipi aliweza zama hizo kufundisha uhakika wa kimatibabu ambao wasomi na usomi wao wameshindwa kugundua uhakika huo ila katika karne ya 21. Wallahi utafiti huu unatoa ushahidi wa dhati kabisa kwamba, dini tukufu ya Kiislamu ni dini ya haki na Mtume wa Uislamu ni kweli kabisa, ni Mtume wa Haki, Mkweli na mwaminifu. Ni wajibu wa kila Muislamu kuona fakhari na kumshukuru mno Mwenyezi Mungu kwa kutuletea mafundisho matukufu kama haya. Naam, waantaswumu khairullakum inkuntuma taalamu. Na huko kufunga ni bora kwenu kama mnajua. Na swuumuu taswihuu, fungeni mpate siha. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.  Walhamdulillahi Rabbil Alamin.

(Visited 92 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!