{ قَالَ سَتَجِدُنِیۤ إِن شَاۤءَ ٱللَّهُ صَابِرࣰا وَلَاۤ أَعۡصِی لَكَ أَمۡرࣰا }

(Musa) Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako.

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


{ قَالَ سَتَجِدُنِیۤ إِن شَاۤءَ ٱللَّهُ صَابِرࣰا وَلَاۤ أَعۡصِی لَكَ أَمۡرࣰا }

(Musa) Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako. [Surah Al-Kahf: 69]
Tumo kwenye Ijumaa nyingine. Kwa taufiki ya Allah nataka kwa pamoja tuangalie somo muhimu sana la kijamii na la kiuongofu ndani ya sura hii iliyohimizwa kusomwa sana hasa siku za Ijumaa.
Nitajitahidi kuandika kwa muhtasari sana ili nisimchoshe msomaji.
Kwa mujibu wa aya hii ya 69 ya sura ya 18 ya Qur’ani Tukufu, Nabii Musa AS alitoa ahadi mbili kwa Nabii Khidhr AS. Mosi na muhimu ni subira na uvumilivu na pili ambayo pia ni muhimu sana, ni heshima na nidhamu.
Ukiangalia lugha iliyotumiwa na Nabii Musa AS kwa mwanafunzi wake, Yush’a bin Nun ambaye katika aya ya 60 ya sura hii tukufu ametajwa kwa sura ya “fataahu” utaona inatofautiana kabisa na lugha yake wakati anazungumza na Nabii Khidhr AS. Kule alizungumza kwa lugha ya mwalimu na hapa anazungumza kwa lugha ya mwanafunzi, na sehemu zote amechunga kikamilifu haki na heshima ya aliyezungumza naye.
Lakini pia ukiangalia lugha iliyotumiwa na Nabii Khidhr AS kwa Nabii Musa AS pia utaona ni jinsi gani mwalimu naye alivyo na wajibu wa kuchunga haki ya wanafunzi wake. Kama ilivyo wajibu kwa mwanafunzi kuchunga heshima ya mwalimu ni wajibu pia kwa mwalimu kuchunga heshima ya mwanafunzi wake.
Kama ilivyo wajibu kwa mwanafunzi kuwa mvumilivu na mwenye subira katika kutafuta ilmu, ni hivyo hivyo ni wajibu kwa mwalimu kuwa mvumilivu kwa wanafunzi wake. Asioneshe kuchoka na asichoke kutafuta njia bora na rahisi zaidi ya kuwafafanulia wanafunzi mpaka waelewe. Awe kioo cha subira na uvumilivu kwao.
Jengine muhimu sana kwa mwalimu na mwanafunzi wake ni kujenga urafiki. Nakuomba rudia tena na tena kuzisoma kwa kina na mazingatio aya za sura ya 18 ya Al Kahf. Hebu angalia aya ya 63, Yush’a bin Nun alipoombwa atoe chakula, anajibu kwa kutumia neno, unaona sigha ya kiurafiki kabisa utadhani si baina ya mwanafunzi na mwalimu ambaye pia ni Mtume wake na akimuasi ataadhibiwa na Allah. Inaonesha jinsi Nabii Musa AS alivyojenga ukaribu na urafiki mkubwa na mwanafunzi wake huyo. (Kuhusu huyu Yush’a bin Nun, tukipata nafasi tutakuja kumzungumzia japo kiduchu Insha’Allah).
Sitaki maelezo yawe marefu. Hapa bado panahitaji maelezo mengine mengi, lakini nadonyoa donyoa tu
Tuchupie kwenye misingi miwili mikuu iliyotumiwa na Nabii Musa kwa ajili ya walimu na wanafunzi, yaani subira na nidhamu. Tujiulize, katika skuli zetu leo hii, zinachungwa haki za walimu na za wanafunzi? Je, misingi hiyo inachungwa?Nakumbuka tulipokuwa wadogo, tuko madarasa ya chini, siku moja tulikuwa tumepanga mstari asubuhi kabla ya kuingia madarasani, mwalimu mkuu aliwaleta mbele wanafunzi wa madarasa ya juu na kutoa adhabu kwa sababu walikuwa wanawadharau vibaya walimu waliokuwa wanatusomesha sisi wa madarasa ya chini. Nakumbuka maneno yake, aliwaambia, kama si walimu wa madarasa ya chini wao kamwe wasingefika madarasa ya juu. Wanafunzi hao walikosa nidhamu, wakatiwa adabu mbele ya wanafunzi wa skuli nzima, likawa fundisho kubwa kwetu hadi leo. Naam, subira na nidhamu ni misingi muhimu sana. Je, unamkumbuka mwalimu wako wa darasa la kwanza au chekechea? Basi angalau muombee dua Ijumaa hii.
Yamebakia maswali mengi bila ya kujibiwa, na maelezo yameshakuwa marefu sana. Miongoni mwake ni kwa nini nidhamu, heshima, subira na uvumilivu umepungua? Kwa nini hufika wakati wanafunzi kupanga njama za kuwadhuru walimu wao? Ni wapi tunapokosea? Utatuzi umo kwenye sura hii ya Al Kahf, lakini bora niishie hapa, isiwe ni kukuchosheni kusoma maelezo marefu.
Mwanafunzi wenu,Ahmed Rashid.

(Visited 9 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!