1. Bismillahi ‘Aliyyun, Ya Ilahi Ya Rahimu
  Bismillahi Qawiyyun, nguvu ni Zako Qayyumu
  Bismillahi Ghafurun, toba ni Kwako Hakimu
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Bismillahi Basirun, unatuona wajao
  Bismillahi Samiun, tusikize viumbeo
  Bismillahi Munirun, nawirisha wakuchao
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia
 1. Rehema Zako Rabana, zeleya kila mahala
  Rehema za Subhana, zenda kwa hata kabwela
  Rehema za Maulana, kwa ‘asi na mcha Mola
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Awali ya Ramadhani, kumi limejaa heba
  Kwa kusoma Qur’ani, na kukithirisha toba
  Wokovu kwa waumini, Rabbi utupe haiba
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Tufunge tukihimidi, rehema zako Rabbana
  Tufunge tukikunadi, turehemu Ewe Bwana
  Tufunge tukiburudi, Amina Rabbi Amina
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Tukitaja jina Lako, tuburudike nafusi
  Tukiona waja Wako, tukukumbuke Mkwasi
  Tukiwa na Peke Yako, tujiepushe kuasi
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Tukwogope hadharani, na zaidi faraghani
  Kubali wetu ugeni, Ilahi Ya Rahmani
  Bila ya Kwako Manani, twende kwa mwengine nani?
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.
 1. Takabali zetu dua, saumu na sala pia
  Waja tumejaa doa, pumzi zinafifia
  Hatutendi kwa kujua, Ya Rabbi twakulilia
  Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.

Na Ahmed Rashid

(Visited 57 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!