Bismillahir Rahmanir Rahim

Historia fupi ya Luqman al Hakim

Kutoka kitabu cha Qasas ul Qur’an cha Ibn Kathir

Luqman ambaye ni maarufu kwa jina la Luqman al Hakim, ni katika waja wema waliotajwa kwa sifa nzuri ndani ya Qur’ani Tukufu. Sura ya 31 ya Qur’ani Tukufu imepewa jina lake. Hili pekee ni muhimu sana kuthibitisha utukufu wa mja huyu mwema.

Mapokezi ya kihistoria yanaonesha kuwa Luqman al Hakim alikuwa Mwafrika na asili yake ni Nubia, Ethiopia. Aliishi karne nyingi nyuma kabla ya kuja Bwana Mtume Muhammad SAW. Aliishi zama za Nabii Daud AS. Naam, ni katika watu watukufu waliotajwa vyema kwa hikma zao kubwa ndani ya Qur’ani  Tukufu. Nasaha nzuri sana alizompa mwanawe, ni miongoni mwa hikma bora zilizotajwa na Qur’ani Tukufu. Tafsiri ya Ibn Kathir na pia kitabu cha visa vya Qur’ani cha Ibn Kathir, ni miongoni mwa marejeo ya historia ya mja huyu mwema ambaye visa vya nyakati mbalimbali za maisha yake vimeenea sana katika lugha mbalimbali hasa za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki. Baadhi ya mapokezi yanasema alikuwa Mtume, lakini mengine yanasema alikuwa mja mwema. Qur’ani haikusema chochote juu ya imma alikuwa Mtume au la, lakini ametajwa kwa sifa za waja wema wenye hikma nyingi, ndani ya Qur’ani Tukufu.

Chanzo cha Luqman kuwa na hikma nyingi

Katika habari zillizonukuliwa kutoka kitabu cha Visa vya Mitume cha Ibn Kathir ni kwamba muda wote Luqman alikuwa anafikiria maumbile na ustadi mkubwa wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Siku moja alipokuwa amelala chini ya mti, malaika alimjia na kumwambia Mwenyezi Mungu anapenda kukupa zawadi, hivyo chagua moja kati ya vitu viwili, imma uwe mfalme au uwe mtu mwenye hikma nyingi. Luqman alichagua kuwa mtu mwenye hikma. Alipoamka alijiona welewa wake umeongezeka kwa sura ya ajabu. Sasa alijiona anaelewa kiundani maana ya vitu vingi, yaliyofichika kwenye dhahiri ya viumbe na elimu na hikma zake ailikuwa zimeongezeka kimiujiza na kwa sura ya ajabu. Hivyo aliporomoka chini kusujudu kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Hayo yamenukuliwa katika kitabu cha Qasas ul Qur’an cha Ibn Kathir chapa ya Dar al Manarah. Tarjama yake ya Kiingereza imetolewa na Ali Sayed al Halawi.

Kutekwa na kuwa mtumwa Luqman

Kwa vile hakuchagua kuwa mfalme, Mwenyezi Mungu alikadiria awe mtumwa kidhahiri, lakini mfalme wa wafalme katika batini. Hivyo alitekwa nyara na kuuzwa kama ilivyokuwa ada na desturi za zama hizo. Hiyo ilimpa fursa ya kutumia vizuri hikma zake. Bwana aliyemnunua alimpenda sana na kimsingi bwana wa Luqman alikuwa mtumwa wa Luqman kutokana na kwamba alikuwa anamsikiliza kila analosema na kumfuata. Hili liliwatia chuki sana watumwa mwenzake na kumfanyia vitimbi vya kila namna kumpaka matope na kumchafulia jina mbele ya bwana wao, lakini muda wote walifeli. Kumenukuliwa visa mbalimbali katika maisha ya Luqman na hikma zake, kama alipotumwa kuchinja kondoo, walipotumwa kwenda kuchuma matunda, alipotumwa kulima ufuta na visa mbalimbali. Mwisho huyu bwana alimwachilia huru Luqman akisema, mtu mwenye hikma nyingi kama huyo, hafai kuwa mtumwa. Nitaweka baadhi ya visa vyake katika website hii ya https://ahramed14.com tukijaaliwa.

(Visited 107 times, 1 visits today)
One thought on “Hikma za Luqman (Sehemu ya Kwanza)”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!