Kisa cha Luqman na matunda ni katika visa vilivyonukuliwa vya hikma za mja huyo mwema wa Mwenyezi Mungu ambaye sura ya 31 ya Qur’ani Tukufu ni ya jina lake. Hadi sasa tumeshazungumzia historia yake fupi na kisa cha kondoo na kuviweka kwenye tovuti hii ya https://ahramed14.com. Leo hapa tumeamua kunukuu kisa cha Luqman na matunda kutoka katika vitabu vya historia.

Miongoni mwa yaliyonukuliwa ni kwamba, siku moja bwana wa Luqman alimtuma aende akachume matunda shambani yeye na watumwa wengine kadhaa. Kama tulivyoona katika sehemu zilizopita, watumwa wengine walikuwa wakimchukia Luqman kutokana na kupendwa mno na bwana wake kuliko wao na kutokana na atia ya hikma aliyozawadiwa na Mola wake.

Mara zote watumwa wengine walikuwa wakifanya njama za kila namna za kumchafulia jina lakini walikuwa wanashindwa. Mara hii pia watumwa wote waliotumwa kwenda kuchuma matunda pamoja na Luqman walipanga kufanya jambo ambalo kamwe Luqman hatoweza kujipapatua na lawama.

Wote walikwenda shambani kuchuma matunda kama walivyoamrishwa. Wakati wakiwa njiani kurejea kwa bwana wao, watumwa wote waliamua kula matunda yote waliyochuma. Walipofika kwa bwana wao halikuwa limebakia hata tunda moja isipokuwa ya Luqman ambaye hakula hata moja. Katika sifa kubwa alizokuwa nazo Luqman ilikuwa ni kutogusa kitu cha haramu hata kitu ambacho uharamu wake uko mbali sana. Akitekeleza kikamilifu na kwa njia bora kabisa kila alilotumwa kufanya.

Walipofika kwa bwana wao, alikasirika mno kuona watumwa wamerejea mikono mitupu, na hakuna hata tunda moja lililobakia.

Watumwa wote walisema, matunda yote yameliwa na Luqman.

Bwana wa Luqman alikasirika, lakini kwa vile alikuwa anajua hikma kubwa za Luqman, hakuchukua maamuzi kwa pupa.

Bwana: Luqman, watu wote hapa wanasema wewe ndiye uliyekula matunda yote. Je, hujui kuwa leo usiku nina wageni muhimu? Kimsingi hebu nieleze, umeweza vipi kula matunda yote hayo peke yako?

Luqman: Seyyid yangu, mimi sikula hata tunda moja. Ninajua vyema kwamba kufanya hivyo ni usaliti. Ni kugusa kitu cha haramu, na mimi sikaribii kitu cha haramu.

Bwana: Sasa utathibitisha vipi kwamba wewe siye uliyekula matunda haya wakati wenzako wote hapa, wanasema ni wewe uliyekula. Hakuna hata mmoja anayepinga?

Luqman: Seyyid yangu tufanyie sote mtihani utaweza kujua ni nani aliyekula matunda na nani hakula.

Bwana: Nitajua vipi nani aliyekula na nani asiyekula? Au unataka nipasue tumbo la kila mmoja wenu? Maana hakuna njia nyingine ya kuweza kujua kilichomo tumboni ila kwa kulipasua tumbo.

Luqman alitabasamu na kusema: Seyyid yangu, unachosema ni sahihi kabisa kwamba matunda yamo ndani ya matumbo ya walioyala. Lakini ili kujua ni akina nani hao, hakuna haja kwako kuwapasua matumbo yao.

Akaendelea kusema: Toa amri sote tunywe maji ya moto. Halafu tuchukue jangwani tutembee kwa miguu.

Yule bwana na kama tulivyosema katika sehemu zilizopita, alikuwa mtumwa wa hikma za Luqman, alikubali ushauri huo wa Luqman licha ya kwamba alikuwa hajui kitakachotokea.

Bwana: Sawa Luqman, lakini nini maana ya kunipa ushauri huu?

Luqman: Seyyid yangu usiwe na haraka. Matokeo yake utayaona waziwazi bila ya hata kuchelewa.

Yule bwana alitoa amri watumwa wote waliokwenda kuchuma matunda akiwemo Luqman wanywe maji mengi ya moto. Baadaye akapanda farasi nyuma akifuatwa na watumwa hao waliokuwa wanatembea kwa miguu jangwani.

Baada ya kupita muda wa kutembea kwa miguu jangwani kwenye joto kali na kutokana na maji ya moto waliyokunwa, Luqman na watumwa wote walianza kutapika. Kila kilichokuwemo tumboni kilitoka nje na kila mtumwa akiazirishwa na matapishi yake.

Heshima za yule bwana zilizidi kuwa kubwa kwa Luqman. Akamuomba msamaha kwa kudhani kwamba angeliweza kutenda kinyume na alivyomuagiza. Naam, wakati mja dhaifu kama Luqman anapoelemezwa tuhuma zisizo na kifani na za uongo, anachotakiwa ni kumlilia Mola wake na kutumia akili na hikma. Ajue kuwa Mwenyezi Mungu Yu pamoja na wanaodhulumiwa. Atambue kuwa anayedhulumiwa, ana Mungu.

(Visited 47 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!