Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limeilalamikia serikali ya Emmanuel Macron ya Ufaransa kwa msimamo wake wa kuihesabu dini ya Kiislamu kuwa tishio la “kigaidi” na kusisitiza kuwa, kuanzia hivi karibuni Paris inauchukulia Uislamu wote kuwa ni tishio kamili la “kigaidi.”

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa “Arab 48” na kumnukuu Kenneth Roth, Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch akisema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la France Press. Amesema, tuna wasiwasi mkubwa kutokana na mbinu inayotumiwa na Ufaransa katika kukabiliana na vitisho vya kigaidi, kwani inaonekana kwamba serikali ya nchi hiyo inauchukuliwa Uislamu wote kuwa ni tishio la kigaidi, wakati hilo ni kosa kubwa sana.

Waislamu wakipita mbele ya Msikiti ulioandikwa maandishi ya chuki dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa

Ameongeza kuwa, licha ya jamii ya Ufaransa kutawaliwa na ada na desturi za kisekula lakini nchi hiyo inapaswa kuheshimu haki za wananchi wake za kuwa huru kutangaza imani na itikadi zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch aidha amesema, kama serikali ya Ufaransa itafanya uafiriti wa kuwaingiza watu wote kwenye kosa la mtu mmoja, basi wananchi wataichukia serikali na jambo hilo litawalazimisha wafuasi wa dini kuendesha kwa siri harakati zao, suala ambalo ni hatari sana.

Roth ametoa matamshi hayo kujibu hatua ya serikali ya Ufaransa ya kuandaa muswada wa sheria mbili zinazozidi kuwakandamiza na kuwanyanyasa Waislamu.

Moja ya sheria hizo ni ya “Usalama kwa Wote” na nyingine ni Mpango wa Kujitenga.

Kifungu cha 24 cha sheria ya usalana kwa wote kimewakasirisha wananchi wa Ufaransa hasa kipengee chake kinachohusiana na waandishi wa habari. Wananchi wa Ufaransa wametangaza hadharani kwamba kipengee hicho kinakandamiza vyombo vya habari. Mashirika ya haki za binadamu pia yamelaani sheria hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch amesema, serikali ya Paris inapaswa kukiri kwamba uandishi wa habari na harakati za wananchi ni mambo halali na ya kimaumbile na haiwezi kuyakandamiza.

(Visited 12 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!