Mpya Kabisa

Waislamu wa Japan

Idadi ya Waislamu na Misikiti yaongezeka kwa kasi nchini Japan

Taarifa kutoka nchini Japan zinasema kuwa, idadi ya raia wa nchi hiyo wanaosilimu na kuingia katika dini tukufu ya Kiislamu inaongezeka sana siku hadi siku. Idadi ya Waislamu wenye asili ya Japan na wasio na asili ya nchi hiyo pia inaongezeka vizuri.

Mtandao wa habari wa “Bol News” umenukuu matokeo ya uchunguzi uliofanywa na taasisi ya Tanada Hirofumi ya Chuo Kikuu cha Waseda nchini Japan yakionesha kuwa, dini ya Kiislamu ndiyo inayokuwa kwa kasi zaidi nchini humo.

Matokeo ya uchunguzi wa chuo kikuu hicho yanaonesha kuwa, idadi ya Waislamu nchini Japan imeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2010 idadi ya Waislamu ilikuwa ni laki moja na 10,000, lakini mwishoni mwa mwaka 2019 idadi ya Waislamu ilipindukia laki mbili na 30 elfu.

Ongezeko hilo limepelekea pia kuongezeka ujenzi wa Misikiti nchini humo na kasi ya ujenzi wa nyumba hizo za Mwenyezi Mungu ni wa kasi kubwa pia.

Muhammad Tahir Abbas Khan, Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Beppu anasema, ongezeko la misikiti nchini Japan linatia moyo na kwamba jumuiya yake inafanya hima kubwa ya kuhakikisha nyumba hizo za ibada zinakuwa karibu na Waislamu kadiri inavyowezekana. Amesema, jambo hilo linawafurahisha Waislamu wote duniani.

Mwaka 2001, wakati Khan alipoelekea Japan akitokea Pakistan, nchi nzima ya Japan ilikuwa na Misikiti 24 huku mjumuiko wa visiwa vya Kyushu vikiwa havina hata Msikiti mmoja.

Sasa hivi lakini anasema, kuna zaidi ya Misikiti 110 katika maeneo yote ya Japan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!