Semina ya kwanza ya maalumu ya kujadili soko la Ulimwengu wa Kiislamu imepangwa kufanyika nchini Iran tarehe 23 mwezi huu wa Juni, 2021 na itahusu soko la biashara la Oman. Semina hiyo itaitishwa na Taasisi ya Qur’ani na Watu wa Vyuo Vikuu nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la habari za Qur’ani, IQNA.

Kituo cha Elimu cha Taasisi ya Qur’ani na Watu wa Vyuo Vikuu ndicho hasa kinachosimamia na kitakachoendesha semain hiyo. Hiyo itakuwa semina ya kwanza katika mfululizo wa semina nyingi zilizopangwa kufanyika nchini Iran kwa ajili ya kujadili njia za kutumia vizuri soko la Ulimwengu wa Kiislamu kuyanufaisha mataifa ya Waislamu.

Taasisi hiyo imekusudia kufanya semina 10 za kujadili kwa kina hali ya kibiashara ya nchi mbalimbali za Kiislamu na jinsi ya kutumia vizuri soko la Ulimwengu wa Kiislamu.

Lengo la kuitishwa mfululizo wa semina hizo ni kutafuta njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika Ulimwengu wa Kiislamu, kubadilishana uzoefu na kuyanufaisha mataifa ya Waislamu katika bidhaa zinazozalishwa kwenye nchi zao.

Semina kuhusu soko la Oman itajikita katika maudhui 11 kuu ambazo ni:

  • Kutoa maelezo jumla kuhusu nchi nzima ya Oman
  • Kutoa maelezo ya kiutaalamu kuhusu uchumi wa Oman.
  • Sifa maalumu za kiutamaduni za wananchi wa Oman, mambo ya lazima na yasiyo ya lazima katika kushirikiana nao kiuchumi na kibiashara.
  • Namna ya kupata visa na kuingia nchini Oman.
  • Kutambulishwa tovuti na marejeo yenye taarifa za kina kuhusu uchumi wa Oman.
  • Kutambulisha vipeumbele vya kiistratijia na muongozo unaohitajika.
  • Kutambulisha fursa za kibiashara na uwekezaji nchini Oman.
  • Namna ya kusajili mashirikika na masuala ya umiliki wa mali nchini Oman.
  • Kujadili ushirikiano wa kielimu, vyuo vikuu na mashirika ya nayotegemea elimu katika uzalishaji (Knowledge Base Companies).
  • Usafirishaji nje bidhaa zinazozalishwa Oman.

Kama tulivyoashiria hapo juu, semina ya kwanza maalumu kuhusu soko la Oman itafanyika kwa njia ya Intaneti siku ya Jumatano ya tarehe 23 mwezi huu wa Juni, 2021 kuanzia saa tatu asubuhi hadi 12 jioni kwa majira ya Tehran, mji mkuu wa Iran. Wataalamu mbalimbali hasa wa vyuo vikuu, wa ndani na nje ya Iran wanatarajiwa kushiriki kwenye semina hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!