Viongozi wa nchi za Kiislamu wamelipa umuhimu mkubwa suala la Palestina katika hotuba zao kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu.

Tovuti ya Umoja wa Mataifa imeripoti habari hiyo na kutoa mfano wa viongozi wa Uturuki, Misri na Qatar katika hotuba zao kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao wamehimiza sana kutafutiwa ufumbuzi kadhia ya Palestina na kutaka Israel iache kuwakandamiza Wapalestina.

Kabla ya hapo Rais Ebrahim Raisi wa Iran alisema katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, Israel ndiyo taasisi kubwa zaidi ya ugaidi wa kiserikali ambayo inatoa maagizo ya kuuawa wanawake na watoto wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina, na hii leo imelifanya eneo la Ghaza kuwa jela kubwa zaidi duniani kutokana na kulizingira kutoka pande zote za angani, baharini na nchi kavu. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kwa upande wake, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alisema katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano kwamba, kadiri dhulma za Israel zinavyoendelea dhidi ya Wapalestina, ndivyo amani na usalama unavyozidi kukosekana Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amesema kwenye hotuba yake kwamba, amani haiwezi kupatikana Mashariki ya Kati bila ya kutatuliwa kadhia ya Palestina. Ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua zinazotakiwa kuboresha hali ya kimaisha ya Wapalestina na kukabiliana na dhulma wanayofanyiwa Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza.

Naye Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Aal Thani amesema kwenye hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2021 kwamba, Israel inapaswa kukomesha uvunjaji wa haki za Wapalestina, iache kukwamisha juhudi za kuundwa nchi huru ya Palestina na ikomeshe pia kuuzingira Ukanda wa Ghaza.

(Visited 11 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!