Mkutano wa kimataifa wa siku mbili uliozungumzia tafsiri za Qur’ani Tukufu umemalizika katika Chuo Kikuu cha Huria cha Allama Iqbal (AIOU), jijini Islamabad, Pakistan.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa DND ambao umeongeza kuwa, mkutano wa kimataifa wa Qur’ani Tukufu uliofanyika katika Chuo Kikuu Huria cha Allama Iqbal (AIOU) umemalizika Ijumaa hii mjini Islamabad, Pakistan kwa nasaha muhimu kwa watafiti waliojikita kwenye tafsiri za Qur’ani Tukufu. Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa ni “Mirengo ya Zama hizi ya Tafsiri za Qur’ani, Misingi na Sheria.”

Mkutano huo umeitishwa na kundi la Qur’ani na Tafsiri la Chuo cha Utafiti wa Kiarabu na Kiislamu na ndani yake kumejadiliwa makala 65 za tafiti zilizotumwa kwenye mkutano huo na watafiti kutoka nchi tofauti duniani, kwa njia ya Intaneti.

Katika kikao cha kufunga mkutano huo, wazungumzaji wamewahimiza watafiti kuzingatia mahitaji ya zama hizi katika utafiti na tafsiri zao za Qur’ani.

Vile vile wafasiri wa Qur’ani Tukufu wamehimizwa kutoa tafsiri za wazi na nyepesi ili juhudi zao hizo zilete uongofu kwa wanadamu hadi siku ya Kiyama. Wazungumzaji wamesema, wanachuoni wa Kiislamu wanapaswa kujua nadharia na tafiti za kisasa kabisa za kielimu na kutumia tajiriba hizo katika utafiti wao wa Qur’ani kwa ajili ya kumletea uongofu mwanadamu wa leo kulingana na mazingira ya zama zake hizi. Dk Ziyaa al Qayyum, mhadhiri wa utafiti wa Kiislamu wa Chuo Kikuu cha Peshawar, Pakistan amesisitiza kuwa, harakati mpya za tafsiri za Qur’ani zinazoendana na zama hizi si tu zina manufaa makubwa kwa Waislamu, kiroho na kivitendo, lakini ufafanuzi wa mafundisho aali na matukufu ya Qur’ani kupitia tafsiri hizo una manufaa makubwa pia kwa wafuasi wa dini nyinginezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!