Bismillahir Rahmanir Rahim.

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Nianza kwa kusema kwamba, wako wanaosema Uzair alikuwa Mtume na wengine wanasema alikuwa mja mwema kama Luqman. Kawaida Qur’ani haitaji kitu isipokuwa kina umuhimu wa hali ya juu kabisa. Hapa lengo si wasifu wa mtu, bali ni suala hilo la Maad na kufufuliwa viumbe. Hivyo mjadala huo wa je alikuwa Mtume au la, tunauacha kama ulivyo.

Uzair ametajwa kwa jina mara moja tu katika Qur’ani Tukufu kwenye aya ya 30 ya Surat al Tauba. Tarjama ya al Muntakhab ya sehemu ya kwanza ya aya hiyo inasema: Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Lakini Uzair ametajwa katika kisa bila ya jina katika aya ya 259 ya Surat al Baqarah kwa mujibu wa wafasiri wa Qur’ani. Aya hiyo inasema: Au kama yule aliyepita karibu na mji uliokwishakuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyoinyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipombainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Naam, Uzair hakuwa mtu mdogo, alikuwa mcha Mungu mkubwa kiasi kwamba Mayahudi walimwita ni mwana wa Mungu kama Wakristo walivyomwita Nabii Isa AS kuwa ni mwana wa Mungu.

Muujiza wa kufishwa kwa karne nzima Uzair

Nanukuu niliyoyaona kwenye maandishi, siongezi langu. Uzair aliishi zama za Nabii Harun AS na ana majina mbalimbali kwa Kiibrania likiwemo la Armia. Wazazi wake walikuwa ni waja wema. Walizaa watoto wawili, mmoja ndiye huyu Uzair mja mwema na mwengine ni Udhra, aliyekuwa muovu, tofauti kabisa na Uzair. Kama kisa cha Habil na Qabil. Uzair aliishi katika mji wa Baitul Muqaddas huko Palestina. Alipotimia miaka 30, Uzair alioa na baadaye alifunga safari akiwa na punda na chakula chake na vinywaji. Akiwa safarini, alipita katika kijiji au mji (neno lililotumiwa na Qur’ani Tukufu ni Qarya). Sehemu hiyo ilikuwa mahame, ilikuwa imesambaratika kabisa, ilikuwa imechakaa kupindukia. Hapo hapo Uzair akakumbuka siku ya kufufuliwa. Akajisemea moyoni, he! Allah ataufufua vipi mji huu. Hakuwa anakanusha ufufuo, bali alikuwa anaona ni kazi kubwa, lakini alikuwa anakiri kwamba Allah ni Muweza wa kila kitu. Pamoja na hayo alishangaa. Utafufuliwa vipi mji uliosambaratika kiasi chote kile?

Mwenyezi Mungu alitaka kuonesha uwezo wake kupitia mja huyu mwema, hivyo aliitoa roho yake kutoka mwilini mwake kwa muda wa karne nzima, naam, miaka 100 kama inavyosema aya ya 259 ya sura ya pili ya al Baqarah. Alipofufuka, Mwenyezi Mungu alimuuliza, umekaa hapa muda gani? Akasema, nahisi ni siku moja, au sehemu ya siku tu, hata siku mbili hazifiki. Mwenyezi Mungu akamwambia bali umekaa hapa miaka 100. Angalia punda wako alivyosambaratika. Lakini pia angalia chakula chako na vinywaji vyao, viko vile vile kama ndio kwanza vimeandaliwa. (Hii haimo katika aya – Na jiangalie wewe mwenyewe na nguo zako, umekaa hapa karne nzima, lakini ni kama uliyepumzika kiduchu tu). Yote kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi sana. Sasa angalia Mola wako anavyofufua. Muangalie punda wako, angalia mifupa tunavyoikusanya, kasha tunaivika nyama, ghafla punda huyo! Na sauti yake ya hoonhoo! Hoonhoo! Panda punda wako na rejea kwa watu wako kuwathibitishia kivitendo nguvu za Muumba wako. Imeelezwa ishara alizotoa mpaka watu wake wakakubali kwamba yeye ni Uzair, Endelea kusoma.

Maisha ya baada ya kufufuliwa Uzair

Baada ya kuamka na kurejea katika mji wake, Uzair aliona mji umebadilika sana. Alianza kutafuta sehemu ilipokuwepo nyumba yake na aliipata. Lakini ili kuwa na uhakika zaidi, alimuuliza bikizee mmoja kipofu, nyumbani kwa Uzair. Yule bibi badala ya kujibu alianza kulia kwani muda mrefu ulikuwa umepita na hakuna yeyote aliyewahi kumuuliza nyumbani kwa Uzair. Alisema, hii ni mara ya kwanza namsikia mtu ananiuliza nyumbani kwa Uzair. Baadaye ajuza huyo alimuongoza Uzair katika nyumba ile ile ambayo alikuwa mwenyewe amekisia kuwa ndiyo nyumba yake.

Jinsi alivyowakinaisha Mayahudi na kukubali kweli yeye ni Uzair

Haikuwa jambo rahisi kwa Uzair kuwathibitisha wakazi wa mji ule kwamba yeye ndiye yule yule Uzair wa miaka 100 iliiyopita. Hivyo Mayahudi walimtaka Uzair awasomee mistari ya Taurati naye aliwasomea Taurati yote kwa moyo. Mwanamke kipofu alimuomba aonesha makarama yake ya kumtibu macho yake. Alimuombea dua na nuru ya macho yake ikarejea. Vile vile aliwaonesha sehemu ambapo baba yake alikifukia kitabu cha Taurati wakati mfalme wa Babilon, Nebuchadnezzar II alipouvamia mji wa Baytul Muqaddas na kufanya mauaji makubwa pamoja na kuchoma moto kila kitu na kuuharibu kabisa. Si hayo tu, lakini pia aliwaonesha alama kwenye bega lake na watu wazima na vizee walioishi na Uzair kabla ya miaka mia moja walikiri kuwa ndiye yeye hasa.

Hatua ya Uzair ya kujua Taurati kwa moyo na kufichua kilipofichwa na baba yake, kitabu pekee kilichobakia cha Taurati, baada ya mfalme wa Babilon, Nebuchadnezzar II kuchoma moto kila kitu huko Baytul Muqaddas, ilikuwa ni zawadi kubwa sana kwa wana wa Israili. Walimuheshimu kupindukia na matokeo yake wakamfanya mwana wa Mungu.

Maelezo zaidi kuhusu Uzair na kuishi kwake Iraq

Naam, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, Uzair alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu katika kizazi cha Bani Israil. Baadhi ya mapokezi yanasema Uzair alikuwa mwanachuoni mkubwa mcha Mungu wa Bani Israil. Aliishi baada ya Nabii Musa AS. Alitekwa nyara baada ya mfalme wa Babilon, Nebuchadnezzar II, au Nebuchadrezzar II, kushambulia mji wa Baytul Muqaddas. Hiyo ilikuwa ni katika miaka ya baina ya 605 BC – 562 BC. Baada ya kutekwa nyara alipelekwa bila ya hiari yake katika mji wa Babil uliokuweko karibu na mji wa Baghdad ya leo huko Iraq. Hata akiwa mjini Babil aliendelea kusomesha na kulea wanafunzi wazuri wa wana wa Israili. Mwaka 458 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS alirejea Orshalem (Baytul Muqaddas) pamoja na wana wa Israili. Alipofika Baytul Muqaddas, kitabu cha Taurati kilikuwa kimepotea kikamilifu na hakuna mwana wa Israili aliyekuwa anakumbuka chochote katika maandishi ya Taurati. Hivyo alifanya kazi kubwa ya kukihuisha na kukirejesha Kitabu hicho kwa wana wa Israili. Uzair alifariki dunia mwaka 430 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS. Hii ndiyo sababu Mayahudi walimpenda kupindukia. Mapenzi yao kwake yaliongezeka na kuchupa mipaka. Kadiri walivyokuwa wanamsifu waliona haitoshi, mwisho wakapindukia mipaka na kumwita mwana wa Mungu baada ya kufariki kwake dunia. Hata hivyo itikadi hiyo haina wafuasi tena katika zama hizi. Hapa chini tunaweka Kuna mjadala mzuri ulionukuliwa katika kitabu cha al Ihtijaj baina ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Mayahudi wa Madina kuhusu Uzair na hoja nzito za Bwana Mtume zilizowaweka mdomo wazi Mayahudi wa Madina kuhusu madai yao kuwa Uzair alikuwa mwana wa Mungu.

Mdahalo baina ya Mtume Muhammad SAW na Mayahudi wa Madina kuhusu Uzair

Ni kutoka kitabu cha al Ihtijaj cha Tabrasi, Juzuu ya Kwanza Ukurasa wa 27.

Makundi matano ya makafiri wa Madina walikusanyana kwa pamoja kwenda kufanya mdahalo na Bwana Mtume Muhammad SAW. Kila kundi liliteua wawakilishi wake watano waliobobea katika elimu za kundi hilo, idadi yao wote ikawa watu 25. Walikubaliana wamvamie kwa pamoja Bwana Mtume kwa hoja nzito nzito na wasimpe nafasi kabisa, kwa ndoto kuwa wangelimshinda kwa hoja. Makundi hayo matano yalikuwa ni Mayahudi, Wakristo, Wamediani (Medians), Wamanichae (Manichaeans) na waabudu masanamu.

Bwana Mtume Muhammad SAW aliwapokea na kujadiliana nao kwa busara ya hali ya juu, upole na maadili ya kiwango cha juu kabisa, na kwa hoja nzito. Aliwapa nafasi ya kutoa hoja zao kwa uhuru na baadaye akajadiliana nao kwa hekima kubwa. Hapa tutanukuu mdahalo baina ya Bwana Mtume SAW na Mayahudi kama ulivyoripotiwa katika kitabu cha al Ihtijaj cha Tabrasi, Juzuu ya Kwanza, Ukurasa wa 27:

Kundi la Mayahudi: Sisi tunaamini kwamba Uzair, Mtume wa Mungu, alikuwa mwana wa Mungu. Tunataka tujadiliane nawe kuhusu suala hili. Kama hoja zetu zitakuwa nzito katika mdahalo huu, na wewe ukakubaliana nasi katika suala hilo, tutakuwa tumekushinda na kama hutokubaliana na hoja zetu, itakuwa ni wajibu kwetu tuendelee kukupinga na kuwa maadui zako.

Mtume Muhammad SAW: Je, mnataka niamini hoja zenu vivi hivi bila ya kuzijadili?

Mayahudi: Hapana

Mtume Muhammad SAW: Basi nipeni hoja zenu za kwa nini mnaamini Uzair ni mwana wa Mungu.

Mayahudi: Ni kwa sababu aliweza kukihuisha kitabu chote cha Taurati wakati kilikuwa kimepotea kikamilifu. Hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na uwezo wa kukifufua isipokuwa yeye Uzair. Hivyo tunaamini kwamba yeye alikuwa ni mwana wa Mungu.

Mtume Muhammad SAW: Kama mantiki na hoja yenu ni hiyo kwamba mnamwita Uzair mwana wa Mungu kwa sababu ameihuisha Taurati baada ya kupotea, kwa nini Nabii Musa ambaye yeye ndiye aliyekuja na hiyo Taurati hamumwiti mwana wa Mungu? Si hayo tu, lakini Nabii Musa alifanya miujiza mingi kuliko Uzair na nyinyi wenyewe mnakiri kwamba Musa ana cheo cha juu zaidi kuliko Uzair, sasa kwa nini hamumwiti mwana wa Mungu, wakati kwa hoja zenu hizi, Nabiyyullahi Musa anastahiki kuwa na cheo kikubwa zaidi ya mwana wa Mungu! Pamoja na hayo, hakuna kati yenu anayesema Musa alikuwa mwana wa Mungu, Swali jengine; lengo lenu la kumwita Uzair mwana wa Mungu ni kumnasibisha na Mwenyezi Mungu kwa nasaba ya baba na mwanawe wa kumzaa kutoka mke aliyeoa? Kama mtadai hivyo, mtakuwa mumemvunjia heshima kupindukia Mwenyezi Mungu Muumba, kwa kumfananisha na viumbe dhaifu wenye viwiliwili, wahitaji na waaliofungwa na mipaka ya dunia.

Mayahudi: Hapana, lengo letu si kuunda nasaba ya baba na mwana baina ya Uzair na Mwenyezi Mungu. Kwani kama ulivyosema, kuamini hivyo kutaishia kwenye ukafiri. Bali lengo leo ni cheo na heshima yake kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Ni kama vile baadhi ya wakati maulamaa wetu wanawaita wanafunzi wao bora, kwa majina ya kijana wangu ili kuonesha hadhi zao ni kubwa zaidi kuliko wanafunzi wengine. Hiyo haina maana huyo ni mwanawe wa kumzaa. Ni vivyo hivyo kwa Uzair mbele ya Mwenyezi Mungu, tunamwita ni mwana wa Mungu kutokana na hadhi yake kubwa mbele ya Muumba.

Mtume Muhammad SAW: Majibu ya hoja yenu hii ni yale yale niliyotangulia kusema. Kama Uzair mnamwita mwana wa Mungu kwa hadhi yake mbele ya Allah, basi Musa AS itabidi mumpe cheo kikubwa zaidi ya mwana wa Mungu kwani nyote mnakiri kwamba hadhi na heshima yake ni kubwa zaidi. Hapa mumepiga mfano wa mwalimu kumwita mwanafunzi wake kwa lakabu ya mwanawe au kijana wake ili kuonesha umuhimu wa mwanafunzi huyo mbele yake ikilinganishwa na wanafunzi wengine. Lakabu zote zinazotumiwa kuonesha heshima na umuhimu wa mtu kwa mtu mwingine, kama vile kumwita mtu ndugu yangu, kaka yangu, baba yangu, mama yangu, mwanangu, Sheikh wangu, Ustadh wangu, Bwana wangu, Sayyid yangu, vyovyote mtakavyotumia, basi lakabu ya Musa inabidi iwe kubwa zaidi. Kama Uzair mnamwita mwana wa Mungu, basi kwa hoja hiyo hiyo je mnaweza kumwita Musa kaka wa Mungu, au Ustadh wa Mungu, au baba wa Mungu? Kwa sababu yeye hadhi yake ni kubwa zaidi kuliko Uzair. Je, mnaweza kumwita Musa hivyo?

Mayahudi hawakuwa na la kujibu, bali walibaki kuduwaa. Mwisho walisema, tupe muda tukafanye uchunguzi na kufikiria zaidi.

Mtume Muhammad SAW: Tab’an kama uchunguzi wenu mtaufanya kwa moyo safi, kwa ikhlasi na kwa insafu, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atakuongozeni kwenye uhakika.

**********

Miongoni mwa vitabu vilivyozungumzia habari hizi ambazo hata hivyo nimenukuu kwa muhtasari ni pamoja na Ibnu Kathir, al Bidaya Wannihaya, Tabari, Daairat al Maarif Lil Qur’an al Karim, Tafsir al Wasit, al Ihtijaj, na vitabu vingi tu.

(Visited 130 times, 1 visits today)
One thought on “KISA CHA UZAIR NA MDAHALO BAINA YA BWANA MTUME NA MAYAHUDI WA MADINA”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!