Maziko ya Sheikh Yaaqub Bagayogo, aliyekuwa amehifadhi Qur’ani nzima na ambaye alikuwa ni maarufu kwa jina la kompyuta ya Qur’ani yamehudhuriwa na idadi kubwa ya Waislamu huko nchini Mali.

Mtandao wa habari wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Sheikh Yaaqub Bagayogo alikuwa maarufu kwa jina la kompyuta ya Qur’ani kutokana na umahiri wake mkubwa wa hifdh na nambari za aya za Kitabu hicho kitakatifu. Si hayo tu, lakini pia alikuwa na umahiri mkubwa wa kujua kurasa za aya za Qur’ani tena kwa haraka sana kuliko kompyuta.

Waislamu wa ndani na nje ya Mali wamesambaza picha zake katika mitandao ya kijamii pamoja na vipande vya video vinavyoonesha umati mkubwa wa Waislamu ulioshiriki katika maziko ya hafidh huyo wa Qur’ani Tukufu aliyekuwa na uwezo wa kipekee kabisa katika hifdh.

Muhammad al Amin, mwandishi na mwanaharakati wa vyombo vya habari wa nchini Burkina Faso amesema, maziko ya Sheikh Yaaqum Bagayogo, mmoja wa ndugu zetu Waislamu wa Mali, yalikuwa makubwa sana. Kutokana na umahiri wake mkubwa katika hifdh, alijulikana kwa jina la kompyuta ya Qur’ani. Amepata taufiki ya kufariki dunia akiwa katika ibada kwani kifo kimemkuta baada ya Sala ya Magharibi na baada ya kutoa mawaidha kuhusu kifo na subira.

Watumiaji wa mitandao wa kijamii wamerusha pia picha na video za hotuba za kipaji hicho cha Qur’ani zinazohusiana na tajwidi na tafsiri ya Qur’ani. Sheikh Yaaqub Bagayoto amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 46. Ameondoka duniani baada ya Sala ya Magharibi katika Msikiti wa Abubakar al Siddiq nchini Mali na baada ya kutoa mawaidha kuhusu kifo na njia za kuvumilia na kusubiri wakati wa misiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!