Kwa mara ya kwanza, Umoja wa Mataifa umepasisha kwa kauli moja azimio la kuzilinda na kuwaunga mkono Waislamu wa Rohingya wa Myanmar na jamii nyinginezo za wachache.

Dhaka Tribune limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, azimio hilo limepasishwa kwa jina la Hali ya Haki za Binadamu za Waislamu wa Rohingya na Jamii Nyingine za Wachache nchini Myanmar na limejikita zaidi katika masuala kama ya uadilifu na haki za binadamu.

Balozi Rabab Fatima, Mwakilishi wa Bangladesh katika Umoja wa Mataifa amesema kuhusu kupasishwa azimio hilo kwamba, hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kupasisha kwa kauli moja azimio kama hilo na hii inaonesha nia ya kweli ya jamii ya kimataifa ya kuumaliza mgogoro wa Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Amma katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Wizara ya Mambo ya Nje ya Bangladesh imesema, muswada wa azimio hilo umewasilishwa mbele ya Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano baina ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Umoja wa Ulaya EU. Katika azimio hilo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeitaka Bangladesh ambayo ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya waliofukuzwa kikatili kwenye ardhi zao nchini Myanmar, ihakikishe Waislamu hao wanapata haki zao kikamilifu kama ambavyo wanashirikishwa vilivyo katika mpango wa taifa wa kupiga chanjo za UVIKO-19 kwa wote, huko Bangladesh.

(Visited 1 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!