Msikiti mmoja katika mji wa Tiznit wa kusini mwa Morocco umevunjiwa heshima vibaya na maadui wa Uislamu wanaoona raha kuwafanyia uafiriti Waislamu mara kwa mara.

Mtandao wa habari wa Le360 umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu wasiojulikana waliuvunjia heshima Msikiti huo mtukufu Jumanne usiku. Msikiti huo unajulikana kwa jina la al Sunna.

Waislamu walipofika Msikitini hapo usiku kwa ajili ya Sala, walikumbana na mazingira ya udhalilishaji mkubwa mbele ya Msikiti huo. Bila ya kuchelewa, wakuu wa Msikiti huo waliwasiliana na maafisa usalama na kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike kuwagundua maadui hao wa dini ya Mwenyezi Mungu na amani na usalama wa Morocco.

Waislamu wakifanya usafi katika Msikiti Mkuu wa Tiznit wa kusini mwa Morocco

Vyombo vingine vya habari vimeripoti kuwa, huo ndio Msikiti mkubwa zaidi katika mji wa Tiznit wa kusini mwa Morocco na kila Ijumaa maelfu ya Waislamu wanashiriki katika Sala ya Ijumaa kwenye eneo hilo tukufu.

Waislamu wamekasirishwa mno na kitendo hicho cha kiuadui cha watu hao na kuwataka maafisa wa serikali waendeshe msako mkali wa kuwagundua na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Viongozi wa Msikiti huo pia wameitaka Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Morocco iweke kamera za kuzunguka Msikiti huo ili kuzuia kurudiwa vitendo hivyo ambavyo hata hayawani hawawezi kuvifanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!