Maafisa wanne wa serikali wamehukumiwa kifungo na faini nchini Somalia baada ya kupatikana na hatia ya kuiba fedha za uma zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya dharura ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

Mahakama ya Kieneo ya Banadir imewapata na hatia maafisa hao wanne wa serikali ya Somalia katika kesi iliyopelekea kufanyika uchunguzi wa wazi wa kugundua jinsi fedha hizo zilivyotumika.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwezi mmoja tu tangu Somalia illiporipoti kesi ya kwanza ya mgonjwa wa corona mwezi Aprili mwaka huu.

Wakati huo Wizara ya Afya ya Somalia ilifichua kuwa, maafisa kadhaa wa serikali walikuwa wanafanyiwa uchunguzi wa kubaini fedha hizo zimepotelea wapi.

Wizara hiyo ilisema mwezi Aprili kwamba, dola baina ya  42,000 hadi 45,000 zimetumika katika mazingira ya kutatanisha. Hata hivyo nyaraka za mahakama zilizotolewa jana Jumatatu hazikusema kila afisa aliyepatikana na hatia kati ya hao wanne, aliiba kiwango gani cha fedha.

Maafisa hao wa serikali ya Somalia wamehukumiwa vipindi tofauti vya kutumikia kifungo jela pamoja na adhabu za kulipa faini za viwango tofauti vya fedha.

Takwimu za karibuni zinaonesha kuwa watu 3,295 wamethibitishwa kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Somalia. 93 kati yao wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huo ulioenea dunia nzima.

(Visited 91 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!