Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Ndugu mmoja ametoa malalamiko na masikitiko yake akisema, sisi ni ndugu watano. Mimi ndiye tajiri kuliko wote. Lakini sijui kwa nini jamaa zangu wanapenda kuwatembelea sana ndugu zangu wengine na kila inapofika zamu ya kunitembelea mimi, hawaji isipokuwa wachache tu. Kila siku utawaona wanawatembelea ndugu zangu wanne. Lakini mimi sioni kutembelewa isipokuwa na jamaa zangu wachache sana tu. Wanafanya uzembe sana, hawanitembelei. Bali wengine huacha kabisa kunitembelea kwa siku kadhaa mpaka huwa hata vivuli vyao sivioni kabisa kana kwamba katika kamusi zao, jina langu halimo kabisa. Wengine wanapokuja kunitembelea huja ni wavivu na wanyong’onyevu kupindukia. Sababu wanazotoa hazikubaliki kabisa. Sijui nifanye nini. Mimi ndiye mkarimu zaidi kuliko ndugu zangu wote kwa kila anayenitembelea. Siwadharau ndugu zangu wala kuwaonea choyo, lakini kila mtu anajua kwamba mimi ndiye mkarimu zaidi kuliko ndugu zangu wote. Wengi wanawashauri jamaa zangu wawe wananitembelea muda wote kwani kuna kheri nyingi watazipata kutoka kwangu na huwa ninawakirimu sana wanaonijia, lakini inasikitisha kuona kuwa, wanazidi kunikimbia na hawasikilizi kabisa mwito wangu. Tatizo ni nini? Kwa nini watu hawa wanafanya ukaidi kiasi chote hiki? Je, mimi si mmoja wa ndugu watano? Kwa nini wananisusia. Kwa nini wananisahau?

Bila ya shaka ndugu yangu utakuwa unauliza, malalamiko hayo yanatoka kwa nani? Ni kutoka kwa kitu chenye thamani kubwa sana, naam, ni malalamiko ya Sala ya Alfajiri.

Kwa kweli yamenifurahisha sana malalamiko na masikitiko haya yenye msisimko na mazuri sana huenda yakawafanya watu wazinduke. Kwa nini sala ni bora kuliko usingizi? Majibu ni kwamba, usingizi ni kuitikia mwito wa nafsi na Sala ni kuitikia mwito wa Allah. Sala ni bora kuliko usingizi kwa sababu usingizi ni sawa na kifo lakini Sala ni uhai. Sala ni bora kuliko usingizi kwa sababu usingizi ni starehe ya mwili na Sala ni starehe ya roho. Sala ni bora kuliko usingizi kwa sababu muumini na kafiri wanashirikiana katika usingizi, lakini Sala haisali isipokuwa muumini. Wanaodumu katika Sala ya Alfajiri ni kundi la waliofuzu, nyuso zao hung’ara, na vipaji vyao humeremeta na nyakati zao hujaa baraka kama wewe ni miongoni mwao, basi mshukuru Allah kwa kukupa taufiki hiyo na kama si katika hao basi muombe Allah akujaalie kuwa miongoni mwao.

Sala ya Alfajiri ni neema bora kabisa, kutekeleza faradhi yake kunakuweka kwenye ulinzi wa Allah na kusali sunna yake ni bora kuliko dunia na vilivyomo na kusoma Qur’ani Alfajiri kunashuhudiwa na Allah na viumbe wema.

ان قرآن الفجر کان مشهودا

 Hakika Qur’ani ya Alfajiri inashuhudiwa daima. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

(Visited 30 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!