Mfawidhi (Mkuu) wa Masuala ya Msikiti Mtukufu wa Makka na Msikiti wa Mtume wa Madina amefungua mashindano ya Qur’ani Tukufu na Hadhith ya wanachuo wa vyuo vikuu vya Haramain.

Gazeti la kila siku la al Yaum la nchini Saudi Arabia limemnukuu Abdul Rahman bin Abdulaziz Al-Sudais, Mfawidhi wa Msikiti wa Makka na Msikiti wa Madina akisema kuwa, mashindano ya hifdh ya Qur’ani Tukufu na Sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW yanafanyika katika kiwango cha taasisi mbili za Msikiti wa Makka na Msikiti wa Madina pamoja na vyuo vikuu vya taasisi hizo mbili.

Amefafanua zaidi kwa kusema, shabaha na malengo ya mashindano hayo ni kuwashindanisha wanachuo katika hifdh ya Qur’ani Tukufu, Hadith na Sira ya Bwana Mtume ili wanachuo wa kike na wa kiume wawe na ukuruba zaidi na Qur’ani na Hadith na kuzifanya nguzo hizo mbili kuwa marejeo yao makuu katika maisha yao.

Al Sudais ameongeza kuwa, miongoni mwa faida za kuitisha mashindano kama hayo ni kulea vijana katika hifdh ya Qur’ani na Hadith na kuongeza uwezo wao wa kuelewa na kutendea kazi mafundisho ya Qur’ani na Hadith.

Ameongeza kuwa, kufanyika mashindano kama hayo kunaleta moyo wa kushindana kwa njia salama wanafunzi wa vyuo vikuu kwa ajili ya kushikamana zaidi na Qur’ani Tukufu na Hadith. Vile vile jambo hilo linaongeza uwezo wa wanafunzi wa kujifunza na kuelewa kwa urahisi zaidi masomo mengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!