Idara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Libya imetangaza habari ya kufanyika mashindano ya Qur’ani kwa ajili ya kushajiisha na kuhamasisha umoja na mshikamano wa kitaifa nchini humo.

Hayo yameripotiwa leo Jumapili na mtandao wa habari wa “eanlibya” ambao umeinukuu idara hiyo ikisema kuwa, ina nia ya kuitisha mashindano makubwa ya kitaifa ya Qur’ani Tukufu na zawadi yake itapewa jina la Tunzo ya Umoja wa Kitaifa.

Kaulimbiu ya mashindano hayo ni aya ya 103 ya Sura ya Tatu ya Aal Imran ya Qur’ani Tukufu ambayo inasema: وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.

Mashindano hayo yanaanza kesho Jumatatu, Aprili 5, 2021 katika Hoteli ya Corinthia ya Tripoli, mji mkuu wa Libya na yatamalizika Jumapili ijayo ya tarehe 11 Aprili, 2021.

Washindani waliopita kwenye mashindano ya mchujo yaliyofanywa na ofisi za mikoa za Idara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Libya ndio watakaochuana kwenye mashindano hayo ya fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!