Wizara ya Wakfu ya Oman imetangaza kuwa, masomo ya kipindi cha joto kali ya Qur’ani Tukufu yamestawi katika msimu huu wa joto kali nchini Oman.

Kwa mujibu wa tovuti ya Shabiba, licha ya Oman kukumbwa na mawimbi ya ugonjwa hatari wa COVID-19 kama ilivyo kwa nchi zote duniani, na licha ya madrasa zote za Qur’ani kufungwa katika mikoa yote ya nchi hiyo ya Kiarabu kama sehemu ya kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona, lakini Idara ya Madrasa za Qur’ani Tukufu ya Wizara ya Wakfu na Masomo ya Kidini ya Oman imechukua hatua za maana za kuendelea na masomo ya Qur’ani katika kipindi hiki cha hatua kali za corona.

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Oman imeelekeza nguvu zake zote kuhakikisha kuwa masomo ya kidini na ya Qur’ani Tukufu hayasimami kwa sababu ya masharti makali ya corona. Miongoni mwa ratiba zilizotiliwa nguvu sana na wizara hiyo ni masomo ya Qur’ani kwa njia ya Intaneti.

Baada ya kufungwa skuli kwa ajili ya mapumziko ya msimu wa joto kali, mwaka huu na kwa mujibu wa kalenda ya kila mwaka, madrasa za Qur’ani Tukufu zilizopasishwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Oman zimepewa jukumu la kuendesha masomo ya Qur’ani Tukufu ya msimu wa joto kali katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ishirikishe wanafunzi 22,241 wa kike na kiume wa rika zote. Masomo hayo yanapaswa kufanyika katika madarasa 1480 kwa njia ya Intaneti.

Kwa upande wake, Hilal bin Hamoud al Riyami, Mkurugenzi wa Idara ya Madrasa za Qur’ani Tukufu ya Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Oman amesema kuwa, lengo la kutolewa masomo hayo ni kutumia vizuri wakati wa wanafunzi na watu wengine katika jamii ya Oman wakati huu wa msimu wa joto kali. Amesema, wanafunzi wanashajiishwa kuhifadhi Qur’ani Tukufu kama ambavyo wanahamasishwa pia wasikatishe njiani.

Vile vile amesema, pembeni mwa masomo hayo, wanafunzi wamewekewa ratiba nyinginezo za kujifurahisha kama mashindano mbalimbali ili kuwajenga kimwili, kiakili na kiimani.

(Visited 41 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!