SWALI

Assalaamu Alaykum. Hebu niweke sawa kwenye tafsiri ya aya hii:

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

Hao watakaoingia Jahannam wadhalilike ni wepi? Wanaojivuna au waoabudu, au wanaoabudu kwa kujivuna?

JAWABU

Bismillahir Rahmnir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Amma kuhusu hiyo aya ya 60 ya Sura ya 40 ya al Ghafir, kwanza mara zote uzuri wa kufasiri aya za Qur’ani na ukamilifu wake, ni kurejea kwenye aya yenyewe ya Kiarabu na kutotosheka na tafsiri zinazotolewa na lugha nyingine. Katika hiyo aya kumetumika neno ‘an. Tab’an kwa kiarabu, hiyo ni harf. Harf hiyo imepambanua vizuri maana.

Jengine muhimu sana katika kufasiri aya za Qur’ani ni kuangalia siyaq yaani mtiririko wa aya yenyewe, za kabla yake na za baada yake. Aya zote hapo zinazungumzia wajibu wa kumwabudu Allah na kwa nini ni wajibu kwa wanadamu wote kumwabudu Yeye Peke Yake. Ndio maana mfasiri maarufu wa Qur’ani, Sahaba wa Mtume, yaani Ibnu Abbas RA alilifasiri neno dua katika hii aya ya 60 kwa maana ya ibada ya kitauhidi. Tab’an wafasiri wengi wamestahabu maana maarufu ya neno dua yaani hilo neno libakie kama lilivyo katika maana yake maarufu ya dua, kwa kutegemea neno ‘astajib lakum’ yaani ahadi ya Allah ya kuwajibu dua zao waja Wake.

Tukirudi tena kwenye harf jar ‘an tutaona kuwa ina maana kadhaa. Miongoni mwake ni kuachana na kitu. Kwa mfano inaposemwa:

  انصرف عنه

maana yake, ameachana naye. Na hiyo ndio maana iliyotumiwa na wafasiri wa Qur’ani hapo katika aya ya 60 ya Surat al Ghafir. Hivyo aya wameifasiri hivi. Hakika wale wanaofanya kiburi wakajiweka mbali na ibada Yangu yaani kuniabudu Mimi Mwenyezi Mungu Peke Yangu, wataingia motoni hali ya kuwa ni dhalili. Ndio maana nikasema, hiyo harf ‘an imepambanua kila kitu hapo.

Amma, lilivyokuja swali lako, inaonesha aliyeuliza amechukulia kwamba, maana ya aya ni Waislamu wanaoabudu Mungu kwa majivuno. Huenda sikuelewa. Lakini kama ni hivyo, maana hiyo iko mbali, ingawa pia sina ilmu ya kujadiliana na wenye mtazamo huo. Hayo ndiyo majibu jumla, ingawa ukisoma tafsiri za Qur’ani utaona kama kawaida wanavyuoni wa tafsiri wamechambua kila kitu mpaka ‘harf sa’ katika hiyo aya pamoja na hilo neno dua na mengineyo. Lakini kwa kiwango cha kujibu swali, naona hapo panatosha.

Niongeze kwa kusema tu kwamba, kwa mujibu wa hadithi mbalimbali za Mtume, kuna sababu nyingi za kutotakabaliwa dua yake mja au waja. Miongoni mwake ni nia mbaya. Hii inajumuisha vitu mbalimbali kama nia ya kumdhuru mtu, nia itokanayo na husda na choyo cha kwa nini fulani na yeye apate, nia mbaya ya kutojua jinsi ya kuomba na nini cha kuomba, nia ya kutomwamini Mwenyezi Mungu, nia ya hebu na mimi nijaribu nione Mungu anaweza kunitimizia kweli haja yangu? Na vitu kama hivyo.

Jengine linalozuia kujibiwa dua ni unafiki. Jengine ni kudharau Sala, yaani kutosali kwa wakati wake. Jengine ni kuwa na mdomo mchafu. Jengine ni kushindwa kuunga udugu. Jengine ni kula chakula cha haramu, kuvaa haramu, kukaa mahala la haramu, kufanya ibada mahala pa haramu, n.k. Jengine ni kuacha kutoa sadaka. Jengine ni kutowapa wengine haki zao kama Zaka, elimu n.k. Alimradi ziko sababu nyingi zimetajwa katika tafsiri ya aya ya 60 ya sura ya 40 ya al Ghafir tunayoizungumzia hapa na aya ya 186 ya Sura ya Pili ya al Baqarah.

Kuna kisa kimenukuliwa kwenye kitabu cha al Ihtijaj kinasema, sharifu mmoja aliulizwa:  Je, Mwenyezi Mungu hakusema, niombeni nitakupeni? Mbona baadhi ya wakati tunawaona watu wana shida kubwa na hawaachi kuomba, lakini Mwenyezi Mungu hawatakabalii. Na baadhi ya wakati aliyedhulumiwa anaomba nusra lakini Mungu hamnusuru? Alimjibu kwa kumwambia, ole wako (kwa kutilia shaka uadilifu wa Mwenyezi Mungu). Hakuna dua ya mtu yeyote ila hutakabaliwa lakini dhalimu dua yake haipokewi mpaka atubu kikweli kweli. Amma mwenye haki hutakabaliwa dua zake kwa kuepushwa na mabalaa bila ya mwenyewe kujua au hulimbikiziwa thawabu zake zimfae siku anapozihitaji zaidi. Na kama jambo aliloomba mja lina madhara kwake, Allah humuepusha nalo.

SWALI

Assalam aleikum. Hapa ndio kwenye suala langu. “Waislam wanaomuabudu Allah kwa majivuno”. Hapa ndio nataka panyooshwe maneno kdg nijiweke sawa.

JAWABU

Mjadala wa swali lako bora ungeupeleka kwenye aya ya 188 ya sura ya tatu ya Aal Imran inayosema:

لَا تَحۡسَبَنَّ ٱلَّذِینَ یَفۡرَحُونَ بِمَاۤ أَتَوا۟ وَّیُحِبُّونَ أَن یُحۡمَدُوا۟ بِمَا لَمۡ یَفۡعَلُوا۟ فَلَا تَحۡسَبَنَّهُم بِمَفَازَةࣲ مِّنَ ٱلۡعَذَابِۖ وَلَهُمۡ عَذَابٌ أَلِیمࣱ

Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia waliyoyafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyoyatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu. [Surat Aal Imran 188]

Hapo pana mjadala mpana. Kwanza je ni furaha yoyote tu, au furaha ya ghururi na majivuno? Je, ni furaha ya matendo yote, au ni furaha ya matendo maovu? Na maswali kama hayo.

Maudhui hiyo imezungumziwa pia kuanzia aya za 261 na kuendelea za Sura ya Pili ya al Baqarah. Zisome aya hizo kwa mazingatio.

Lakini pia hapa nimekumbuka ile audio ya aina saba za nafsi niliyowahi kuirekodi na kuiweka humu mtandaoni. Inapatikana katika link hii hapa chini ambayo mtu anaweza kudownload na kuwa nayo kwenye simu au Tab au Laptop au ngamiza yake: https://ahramed14.com/aina-saba-za-nafsi/

Wanadamu wengi wana daraja ya chini kabisa ya nafsi, nafsi ya akina Qarun, Firauni, Abu Lahab na wengine kama ile iliyotajwa katika aya ya 188 ya Surat Aal Imran. Waislamu wengi wana daraja ya pili ya nafsi, wengine hata hatufikii kwenye nafsi ya kutoa ilhamu sisemi tena daraja ya nne ya nafsi yenye tuo na tatu za juu yake. Mtume yeye ana daraja ya juu kabisa, nafsi iliyo kamili kwa kiwango kilichokusudiwa na Allah, sisi wengine ndio kwanza tunajikongoja kwenye nafsi za kwanza na pili. Ni wepesi wa kukasirika, wepesi wa kukata tamaa, wagumu wa kutoa, wingi wa majivuno, wachache wa kutenda mema, mabakhili na hicho tunachokitoa tunakifanyia majivuno na masimbulizi. Mtu anaweza kuwa mcha Mungu mbele ya macho ya watu, lakini kama atapita sehemu hakusalimiwa na mwanafunzi wake, jirani yake, mtu anayemfadhili, utamuona anakasirika na kusema moyoni “wema wote niliomfanyia, haya ndiyo malipo yake?” Hizo ni katika daraja za chini kabisa za nafsi. Tujitahidi jamani. Viburi viko vya aina mbili, kiburi cha mwenye kitu na kiburi cha asiye na kitu. Vyote ni vibaya na vinatokana na nafsi ngonjwa, ya chini kabisa inayopaswa kuonewa huruma. Hilo ndilo chaka la ibilisi. Mungu atupe taufiki ya kupambana na nafsi hiyo maana hata tukifanya jema gani na ibada gani, lakini kama tutaendelea kuwa na nafsi hiyo ambayo inapenda sifa hata kwa jambo ambalo nafsi hiyo haikutenda basi itakuwa ni bure. Hii ndiyo jihadi kubwa. Hata tukijitia pepo mwehu na mpumbavu, nafsi zetu zitatusuta. Nakuomba isikilize tena na tena hiyo audio na wakumbushe na wengine huenda akatokea japo mmoja akafanya juhudi za kuiondoa nafsi yake mahala ilipo na kuipandisha daraja ya juu zaidi.

Amma tukirudi kwenye aya niliyokuomba yuislamu ya 188 ya sura ya tatu, napenda kusema kuwa, ni furaha ya majivuno na kiburi ndiyo inayozungumziwa katika aya hiyo ya 188 ya Surat Aal Imran. Kwa daraja la kwanza aya hiyo inawahusu makafiri hasa unapoangalia siyaq na mtiririko wa aya yenyewe na kibwagizo chake. Lakini inawahusu pia Waislamu wanaofanya viburi na majivuno katika ibada zao. Kiburi na majivuno ni cha nafsi hatari na ya daraja la chini kabisa hata kikifanywa na mwanachuoni aliyemaliza vitabu vyote vya ilmu au mtu ambaye paji lake limepiga suguru kwa ibada. Ninapenda sana kuzungumzia madhara ya nafsi hii hatari kwani kupambana nayo ni jihadi kubwa kuliko zote.

Naam, kiburi cha mwenye nacho na cha asiye nacho vyote viwili havifai! Kiburi cha kutokuwa tayari kuomba radhi ni kibaya pia. Majivuno ya kwamba mimi sitoki msikitini, kila siku niko darsa, Hijab na kofia siivui, nitakuwaje sawa na yule, ni kiburi na majivuno mabaya sana. Tumeshasema mengi, lakini hayatoshi kama hatutasema pia njia za kupambana na nafsi hiyo.

MUULIZAJI

Nimeona nichukue hapa, ingawa umeniambia nianzie Aya 216 lkn naona kwenye Aya hii ni munasaba wa jibu la swali langu.

یَـٰۤأَیُّهَا ٱلَّذِینَ ءَامَنُوا۟ لَا تُبۡطِلُوا۟ صَدَقَـٰتِكُم بِٱلۡمَنِّ وَٱلۡأَذَىٰ كَٱلَّذِی یُنفِقُ مَالَهُۥ رِئَاۤءَ ٱلنَّاسِ وَلَا یُؤۡمِنُ بِٱللَّهِ وَٱلۡیَوۡمِ ٱلۡـَٔاخِرِۖ فَمَثَلُهُۥ كَمَثَلِ صَفۡوَانٍ عَلَیۡهِ تُرَابࣱ فَأَصَابَهُۥ وَابِلࣱ فَتَرَكَهُۥ صَلۡدࣰاۖ لَّا یَقۡدِرُونَ عَلَىٰ شَیۡءࣲ مِّمَّا كَسَبُوا۟ۗ وَٱللَّهُ لَا یَهۡدِی ٱلۡقَوۡمَ ٱلۡكَـٰفِرِینَ

Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyochuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.

Sawasawa, kwa maana hiyo wale ambao wanafanya Ibada zao lkn kwa Ria na Majivuno hawatopata chochote, kwa Allah au hawatolipwa kitu, amali zao hazina makusudi ya Allah.

JAWABU

Shukran kwa kuzipitia hizo aya. Nilitaka uanzie juu ili upate picha kamili. Hivyo kutumika maneno “Enyi mlioamini” katika aya hiyo hapo juu, inaonesha ugonjwa huu hatari hauko kwa makafiri tu, bali uko pia kwa Waislamu.

Tuendelee na maudhui yetu kwa kukumbusha kuwa, furaha ya mtenda ibada ambayo haina ria, wala kiburi, wala majivuno, inatakiwa na ni jambo zuri sana. Kwa mfano mtu amewapa wenzake nguo za sikukuu, moyo wake ukafurahi kwa kuona furaha za watoto wale, bila ya kujionesha wala majivuno, bali kwa kumshukuru Mungu kwa kumpa taufiki hiyo ya kutia furaha katika nyoyo za waja wa Mungu, hicho ni kiwango kizuri cha kuilea nafsi na hiyo ni moja ya njia za kupambana na nafsi ngonjwa. Msaada wowote hata wa maneno unaotolewa kwa ikhlasi, ni njia ya kuilea vizuri nafsi. Kwa hivyo sehemu ya kwanza ya furaha iliyozungumziwa katika aya ya 188 ya Surat Aal Imran ina pande mbili, sahihi na batili. Sehemu ya pili ya furaha, yaani mtu kupenda sifa kwa jambo asilotenda, nayo ina sura mbili. Moja na ambayo ni pana zaidi, ni upande wake wa batili. Haufai kabisa. Lakini ina pia upande chanya, positive, nao ni kwamba kama itatokezea kwa bahati, mtu akasifiwa kwa wema hata ambao hajautenda, anatakiwa ajipinde kutenda wema huo, ili maneno ya waliomsifu, yasiwe ni uongo. Hiyo ni njia nyingine ya kuilea na kuitibu nafsi ngonjwa.

Njia nyingine ni istighfar na kuomba msamaha kwa wingi. Hiyo “istikbar an ibadati Llah” inalenga pia hapo. Njia nyingine ya kuitibu nafsi ya daraja la chini, ni kutangulia mtu kuilaumu mwenyewe nafsi yake. Ukifanya kosa jilaumu mwenyewe, usiwasukumie wengine lawama maana tabia hiyo ni ya nafsi mbovu. Dhikr kwa wingi, ni silaha nzuri ya kupambana na nafsi ya daraja la chini na madaraja mengine. Jipangie mwenyewe uradi au nyuradi zako, ziwe ni siri baina yako na Muumba wako, hata mumeo, mkeo, kaka yako, dada yako, shangazi yako, chichi yako, mjomba wako na mwanadamu yeyote asijue, nyuradi hizo zitakusaidia sana kila pale pepesi za shetani zinapokukaribia.

Katika wema pia, vivyo hivyo. Katika kutoa na kusaidia pia ni hivyo hivyo. Tufanye kwa ikhlasi. Tusiwe kama yule waliyemuona msikitini amejipinda kwa kusali na kuvuta nyuradi na kusoma Qur’ani.  Watu waliopo pembeni wakasemezana, Masha’Allah huyu bwana ni mcha Mungu sana, amejipinda kikamilifu kwa ibada. Yule bwana mpenda sifa akakatisha Sala, akawageukia na kuwaambia, na kufunga pia nimefunga leo!

Kiujumla ziko njia nyingi za kuilea nafsi na kuipandisha daraja ya juu zaidi. Sisi si maasumu, huenda hatuwezi kufikia hata daraja ya nne, lakini tunaweza kuvuka kigingi cha kwanza tukaingia hadi daraja ya pili na ya tatu. Zote hizo hatutakosa fungu kwa Muumba. Tujipinde jamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!