Maulamaa wa India wametoa tamko la pamoja na huku wakilaani unyama unaofanywa na Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na Ghaza, wametaka kuungwa mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na kushinikizwa Israel ikomeshe uadui wake.

Shirika la habari la WAFA la Palestina limenukuu sehemu moja ya taarifa hiyo ya maulamaa wa India wakisema: “Tunaamini kwamba uadui huu ni sehemu ya mbinu za kigaidi za Israel za kutaka kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao kwa kutumia mabavu na kuwaweka sehemu hizo walowezi wa Kiyahudi, suala ambalo ni uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa.”

Maulamaa wa India pia wamesema: “Mashambulio ya kidhalimu na ya kikatili yanendelea hivi sasa kwa ajili ya kuwafukuza Wapalestina katika eneo la Sheikh Jarrah huko Quds, huku wahanga wakuu wakiwa ni wananchi wa kawaida kama vile watoto, watu wasiojieweza na wanawake. Huo ni ukatili mkubwa wa kinyama unaofanywa na Israel kwa kiwango kikubwa mno. Kuwafukukza watu katika eneo lao ni uvunjaji wa wazi wa misingi yote ya haki za binadamu.”

Aidha maulamaa hao wakubwa wa India wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba, njia iliyotumiwa na Israel ya kuvamia Msikiti wa al Aqsa na kuwashambulia Waislamu waliokuwa wanasali (tena ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) imewaumiza mno Waislamu wote duniani kwani Msikiti wa al Aqsa ni eneo la tatu lenye utukufu zaidi kwa Waislamu na ni eneo lenye uhusiano wa moja kwa moja na hisia zetu za kidini. Hivyo watu wote duniani wanapaswa kulaani vikali vitendo vya kinyama vya Israel dhidi ya eneo hilo takatifu. Maulamaa hao pia wamesema, unyama wa Israel wakati huu wa ugonjwa wa COVID-19 unafanyika kama sehemu ya kujiimarisha kinyume sheria na ni jinai hatari dhidi ya ubinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!