Mesut Özil, mchezaji nguli wa timu ya Arsenal ya nchini Uingereza ametumia aya ya Qur’ani Tukufu kutoa mwito kwa Waislamu kukabiliana kwa busara na hekima na maadui wa Uislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, Özil ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka sana duniani hasa barani Ulaya na vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika sula hilo.

Vile vile amesema, tunapaswa kukabiliana na wimbi hilo la uadui dhidi ya Waislamu na Uislamu kwa namna ambayo haitopelekea kuongezeka vitendo hivyo.  Ametoa mwito wa kutumika busara na hekima katika kuzima moto huo wa chuki dhidi ya Uislamu.

Fahali huyo wa timu ya wabeba bunduki ya Arsenal ametumia aya ya 34 ya Sura ya 41 ya Fuswilat kutilia nguvu maneno yake. Aya hiyo inasema:  Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.

Miaka miwili iliyopita pia, mchezaji huyo wa Arsenal raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki alilalamikia pia uadui wanaofanyiwa Waislamu nchini Ujerumani.

Mesut Özil wakati huo alikuwa anachezea timu ya taifa ya Ujerumani. Alisema, wakati tunaposhinda mechi fulani, wananiita Mjerumani, lakini wakati tunaposhindwa katika timu ya taifa ya Ujerumani, wananiita mhamiaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!