Mchungaji mmoja wa Nigeria ambaye hivi sasa anaishi Minnesota Marekani ameamua kuukarabati Msikiti wa miaka 60 huko Ikire, katika jimbo la Osun, kusini magharibi mwa Nigeria ili kulipa fadhila alizofanyiwa na Waislamu wakati alipokuwa mdogo.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa AboutIslam ambao umemnukuu mchangiaji mmoja wa mitandao ya kijamii, anayeitwa Bakara Adegboyego akisema wiki hii katika ukurasa wake wa Facebook kwamba, Msikiti huo wa Ikire uliko katika makutano muhimu ya barabara umekarabatiwa na mchungaji Oluwaseun Alabi.

Mwenyewe mchungaji huyo amesema, wakati walipokuwa wadogo, walipitisha muda mzuri na wa furaha sana na Waislamu katika mji wa Ikire huko Irewole, katika jimbo la Osun nchini Nigeria kwenye maieneo ya Msikiti wa Alatise, mjini Ikire bila ya kubaguliwa.

Msikiti wa mji wa Ikire uliokarabatiwa na mchungaji nchini Nigeria ili kulipa fadhila za Waislamu

Adegboyego ameweka pia picha za Msikiti huo kwenye ukurasa wake wa Facebook na kupongezwa sana na watu mbalimbali.

Imam Mkuu wa mji wa Ikire, Alhaj Yunus naye ametoa maoni yake kuhusu hatua ya mchungaji Oluwaseun Alabi ya kuukarabati Msikiti huo na kusema kuwa, Uislamu hauna uadui na mtu yeyote asiyeifanyia uadui dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Katika sehemu moja ya ujumbe wake, mchungaji Alabi pia amesema, tumekulia kwenye jamii ya watu ambao waliishi bila ya chuki za kidini tofauti na hivi sasa.

Nigeria ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu magharibi mwa Afrika.

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA katika ripoti yake linasema, asilimia 50 ya raia wa Nigeria ni Waislamu huku shirika la utangazaji la BBC likisema kuwa idadi hiyo ni zaidi ya asilimia 50. Waislamu wenyewe wa Nigeria wanasema kuwa, takwimu zao zinaonesha kwamba Waislamu ni wengi mno na idadi yao inazidi kwa mbali hayo makisio yanayotolewa na nchi za Magharibi.

(Visited 86 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!