Jengo la Makumbusho la Muscat, mji mkuu wa Oman ni hazina ya nakala za thamani kubwa za Misahafu iliyoandikwa kwa mkono na mabingwa wa Khat wa Oman. Mabingwa hao walidhihirisha vipawa vikubwa na jinsi walivyotabahari katika uandikaji wa Qur’ani Tukufu na kila mmoja alifanya juhudi zake zote kuonesha kipaji chake cha hali ya juu katika kazi hiyo tukufu. Misahafu hiyo imeandikwa kwa Khat jamili za kuvutia, kurasa zake zimepambwa kwa ulimbwende wa hali ya juu na majalada yake ni ya kipekee ambapo kila msahafu unamwambia mwenzake nipishe, mimi ninapendekeza zaidi.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al Watan wa nchini Oman, jengo la Makumbusho ya Taifa ya Oman ni hazina ya vitu vya thamani kubwa ambavyo humvutia kila anayetembelea makumbusho hayo. Makumbusho hayo ni dhihirisho la mchango mkubwa wa Waomani katika ilmu na utamaduni. Ndani ya makumbusho hayo zinapatikana pia nakala zenye thamani kubwa za Qur’ani Tukufu zenye nakshi za kipekee. Ni fakhari kwangu kupata taufiki ya kusema yafuatayo hapa chini kuhusu kazi hiyo adhimu, naam kazi ya kukitumikia Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani.

Ukumbi wa Adhamat al Salaam

Ukumbi wa Adhamat al Salaam wa jengo la Makumbusho ya Taifa la Oman mjini Muscat umejaa turathi zinazomvutia kila mtazamaji. Miongoni mwa turathi hizo zenye thamani kubwa ni nakala za Qur’ani Tukufu zinazodhihirisha kipaji kikubwa cha Waomani katika fani ya Khat na mchango wao mkubwa wa kielimu na kiutamaduni katika Uislamu.

Jengo la Makumbusho ya Taifa Muscat Oman

Katika Makumbusho yaliyohifadhi nakala zilizoandikwa kwa mkono za Wizara ya Turathi za Kiutamatuni na Utalii ya Oman, kuna misahafu ifikayo 200. Muhammad al Tarshi, Mkuu wa Kitengo cha Kusajili Nakala Zilizoandikwa kwa Mkono anasema: Kati ya Misahafu hiyo ambayo ni fakhari ya kisanii ya ulimwengu wa Kiislamu, zinapatikana nakala za Qur’ani zilizotumia ustadi wa hali ya juu wa ufundi wa kifinyanzi wa kuchanganya kiutaalamu udongo na mimea. Nakshi za Misahafu hiyo zimechorwa kwa ustadi wa hali ya juu kiasi kwamba mtu anapoziangalia hudhani si nakshi zilizoandikwa kwa mkono. Rangi zake zimechanganywa kwa ufundi wa hali ya juu na zinang’ara kwa namna ambayo huyavutia kiaina yake moyo na macho ya kila anayeziangalia. Kiujumla mabingwa wa uandishi wa Khat wa Oman walidhihirisha vipaji vyao vya kila namna wakati walipoandika kwa mkono Misahafu hiyo.

Iliandikwa kwa tabu, hima na hofu

Amma suala jingine tunalopenda kusema hapa ni kwamba, mwishoni mwa nakala zote hizo za Qur’ani, kuna kurasa nzuri za kisanii zenye beti za mashairi kutoka kwa waandikaji wa Misahafu hiyo. Sehemu kubwa ya mashairi hayo yanazungumzia juhudi na tabu walizopitia. Pia yanazungumzia wasiwasi na woga mkubwa waliokuwa nao waandishi, wakihofia kufariki dunia kabla ya kumaliza kuandika. Kipande kimoja cha beti hizo kwa lugha nyepesi unaweza kusema kinasomeka hivi: Hakuna mwandishi yeyote atakayebakia milele, lakini alichokiandika kitabakia milele. Ikhlasi kama hii ya kupigiwa mfano ndiyo iliyonisukuma niweke makala hii hapa.

Kama Waislamu wengine, Waomani nao wametoa mchango mkubwa katika ilmu na utamaduni wa Kiislamu

Mus’haf al Sindi

Msahafu wa al Sindi ni turathi iliyobakia hadi leo kutoka kwa mwandishi wa Khat wa Kiomani, Muhammd bin Fadhil al Sindi. Msahafu huo uliandikwa mjini Muscat mwaka 1179 Hijria. Sasa hivi Msahafu huo unahifadhiwa katika Maktaba ya Wizara ya Turathi za Kiutamaduni ya Oman.  Msahafu huo umekhitimishwa na aya ya 115 ya Sura ya 6 ya al An’am ambayo inasema:

وَ تَمَّتْ کَلِمَةُ رَبِّکَ صِدْقاً وَ عَدْلاً لا مُبَدِّلَ لِکَلِماتِهِ وَ هُوَ السَّميعُ الْعَليمُ

Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye Ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Aya hiyo imeandikwa ndani ya fremu ya duara ambayo usuli (background) yake ni buluu na imenakshiwa kwa rangi nyekundu, njano na nyeusi.

Juhudi kama hizi za kuandika Misahafu kwa mkono zinaonesha jinsi Waislamu wanavyokithamini mno Kitabu hiki kitakatifu tangu kale

Mbinu zilizotumika

Moja ya mbinu zilizokuwa zikitumika sana katika uandikaji wa Qur’ani Tukufu kwa mkono katika enzi za kale nchini Oman ni ile ya kutumia neno “ta’qibah – تعقيبة.” Neno hilo lilikuwa linatumiwa mwishoni mwa kila ukurasa wa kulia na mwanzoni mwa ukurasa unaofuatia. Neno hilo lilikuwa linatumika kwa maana ya kumuonesha msomaji kuwa hajafika mwisho bali aya zinaendelea. Hiyo ilikuwa ni aina fulani ya kutia nambari kurasa za Misahafu hiyo. Katika enzi za kale, waandishi walikuwa wanatumia sana mbinu hiyo. Mwandishi alikuwa anatumia neno hilo na kuongeza neno moja au mawili ya ukurasa unaofuata, chini ya mstari wa mwisho wa ukurasa, ili kurasa za kitabu zisiparaganyike.

Msahafu wa kale zaidi

Al Tarshi amesema, alipoifanyia uchunguzi Misahafu ya karne za 11 hadi 14 ya nchini Oman ameona kwamba moja ya Misahafu ya kale zaidi ambayo ipo hadi leo ni ule ulioandikwa nchini Oman mwaka 1054 Hijria. Umeandikwa na Salim bin Rabii bin Rashid al Bahlawi. Sasa hivi nakala ya Msahafu huo inahifadhiwa katika Maktaba ya Wizara ya Turathi na Utamaduni ya Oman.

Hata hivyo kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al Watan, kuna Msahafu mwingine wa kale zaidi ambao unahesabiwa kuwa ndio Msahafu wa zamani zaidi uliopo hivi sasa nchini Oman. Huo ni ule Msahafu ulioandikwa kwa mkono na mmoja wa mabingwa wa Khat wa Oman. Msahafu huo unapatikana katika Makumbusho ya Abi al Hakam Ahmad bin Abdullah al Harithi. Uliandikwa mwaka 1028 na bingwa wa Khat, Ahmad bin Abdullah al Khalili.

Aina za Misahafu ya kale Oman

Vile vile Muhammad al Tarshi anasema kuhusu utafiti aliofanya juu ya Misahafu iliyoandikwa kwa mkono kwamba, Misahafu hiyo imegawanyika sehemu mbili. Sehemu moja ni Misahafu iliyo kamili na nyingine ni isiyo kamili. Misahafu kamili ni ile ambayo majina ya waandishi wake yanajulikana na kurasa zake ni kamili. Idadi yake katika makumbusho hayo ni takriban nakala 50. Amma Misahafu isiyo kamili ndiyo mingi. Inafika 250. Hii ni ile Misahafu ambayo waandishi wake hawajulikani, haina majalada yake ya asili na kurasa zake ni pungufu kutokana na kutumika sana au kurowa au kuchanika na sababu nyinginezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!