Waziri Mkuu wa Bangladesh amefungua misikiti 50 mipya kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa Arab News ambao umeongeza kuwa, kufunguliwa misikiti hiyo na Waziri Mkuu wa Bangladesh ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa vitu mbalimbali utakaogharimu dola bilioni 1. Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2017 nchini Bangladesh.

Mradi huo unajumuisha ujenzi wa misikiti 560 ambayo itakuwa na sehemu mbalimbali za mikutano, elimu na shughuli nyinginezo za kijamii.

Waziri Mkuu wa Bangladesh Bi. Sheikh Hasina, ambaye anajulikana pia kwa jina la kuolewa la Sheikh Hasina Wazed, amefungua misikiti hiyo 50 kwa njia ya video na Intaneti. Wakati akifungua misikiti hiyo amesema, ana matumaini makubwa kuwa misikiti hiyo itatumika vizuri kuonesha sura nzuri na halisi ya Uislamu isiyo ya misimamo mikali na ya kuwakufurisha Waislamu wengine.

Waziri Mkuu huyo wa Bangladesh pia amesema, sote tumeona jinsi baadhi ya watu wanaotumia jina la dini kufanya vitendo vya kigaidi. Kuua watu wasio na hatia na kueneza chuki kunaharibu sura ya Uislamu. Watu wote wakiwemo wanasiasa, watu katika jamii na maulamaa wana wajibu wa kufanya juhudi zao zote kung’oa mizizi ya ugaidi. Inabidi watu waelewe kuwa, mtu yeyote hawezi kuingia peponi kwa kudhulumu roho za watu wengine. Misikiti mingine iliyobakia na ambayo inajengwa chini ya mradi huo mkubwa wa taifa, itafunguliwa katika siku za usoni huko Bangladesh kwenye minasaba mbalimbali ya kidini na kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!