Vyombo mbalimbali vya habari duniani jana Jumatatu vilitangaza kuwa, baada ya kupita masaa manne ya kukwama kutoa huduma shirika la mtandao wa kijamii la Facebook, mkuu wa shirika hilo, Mark Zuckerberg amepoteza dola bilioni 7 za utajiri wake.

Russia Today imetangaza kuwa, wafanyakazi wa Facebook walishindwa hata kuingia ofisini kutokana na kukwama kadi za o za mlangoni.

Chombo hicho cha habari ya Russia kimetangaza pia kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba zaidi ya taarifa bilioni 1.5 za watumiaji wa Facebook zimepigwa mnada na wadukuzi.

Vile vile kwa mujibu wa data za “Privacy Affair” taarifa za watumiaji wa Facebook zilizodukuliwa na kupigwa mnada ni pamoja na jina la mtumiaji, b-pepe yake yaani Email, nambari ya simu, mahali alipo, jinsia yake kama ni mwanamme au mwanammke n.k.

Data hizo mpya zinahusiana na mwaka huu wa 2021. Hata hivyo shirika la Facebook linadai kuwa, ni jambo lililoko mbali kuweza shirika hilo kudukuliwa na wadukuzi.

Ijapokuwa wakuu wa Facebook wamekanusha madai ya kujipenyeza wadukuzi katika mifumo yake ya mawasiliano lakini afisa mmoja wa Marekani hivi karibuni kabisa aliiambia televisheni ya Sky News kwamba kulikuwa na uwezekano shirika la Facebook na tovuti nyingine nyingi kudukuliwa na wadukuzi. 

Mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp ina mabilioni ya watumiaji

Facebook ulikuwa ni mtandao wa kwanza kabisa wa kijamii ambao watumiaji wake walipindukia watu bilioni moja. Hivi sasa mtandao huo una watumiaji zaidi ya bilioni 2 na milioni 850 amilifu (active) kila mwezi.

Mbali na Facebook yenyewe ya asili, shirika hilo hivi sasa linamiliki pia mitandao mingine mikubwa ya kijamii ya WhatsApp, Instagram na Facebook Messenger.

Ikumbukwe pia kuwa mwezi Juni 2021, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliupiga marufuku mtandao wa kijamii wa Twitter nchini humo. Tangu wakati huo idadi kubwa ya wananchi wa Nigeria wamemiminika upande wa Facebook na mitandao yake tanzu, huku wengine wachache wakiendelea kutumia mtandao wa Twitter kupitia vpn.

Nigeria ina karibu watumiaji amilifu (active) milioni 33 wa mitandao ya kijamii tangu mwezi Januari mwaka huu. WhatsApp ndio mtandao maarufu zaidi unaotumiwa na watu wengi nchini Nigeria. Kwa mujibu wa “Statista” kuna zaidi ya watumiaji milioni 90 wa WhatsApp nchini Nigeria pekee.

Takwimu hizo zinaonesha pia kuwa sasa hivi karibuni asilimia 61.4 ya Wanigeria wanatumia Twitter, asilimia 86.2 wanatumia Facebook, asilimia 81.6 wanatumia YouTube, asilimia 73.1 wako kwenye Instagram na asilimia 67.2 wanatumia Facebook Messenger.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!