Msikiti mkubwa zaidi huko Scotland umeamua kuwa kigezo cha kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa na kulinda tabianchi kupitia kutumia nishati ya jua katika matumizi yake.

Mtandao wa Islamic Relief umeripoti habari hiyo na kuongezakuwa, kulindwa mazingira ni jambo muhimu sana katika Uislamu. Kwa mtazamo wa Uislamu, kuna uhusiano mkubwa baina ya mwanadamu, Mwenyezi Mungu na viumbe vyake vyote ikiwemo mimea na wanyama.

Hatua ya Msikiti huo mkubwa zaidi wa Scotland ya kutumia nguvu za jua ni ubunifu mzuri wa kulinda mazingira na hatua hiyo imekuja sambamba na kufanyika Mkutano wa Kukabiliana na Uchafuzi wa Hali ya Hewa ulioitishwa na Umoja wa Mataifa huko Scotland.

Irfan Razzaq, Katibu Mkuu wa Msikiti Mkuu wa Glasgow huko Scotland amesema, mwandamu ni khalifa wa Mwenyezi Mungu ardhini na hilo ni jukumu letu la kimaadili ambalo linatuwajibisha kufanya juhudi zetu zote kuhakikisha tunalinda usalama wa sayari ya dunia na viumbe wote wanaoishi ndani yake.

Katika mradi huo kutatumia sahani 130 za sola yaani za kupokea mionzi ya jua na inatarajiwa kuwa kwa mwaka utapunguza uzalishaji wa gesi chafu za CO2 kwa takriban kilo 18,000.

Amesema, zaidi ya Misikiti 1500 kote Scotland inaweza kutoa mchango mkubwa wa kulinda mazingira kupitia kutumia nguvu za jua katika uendeshaji wa misikiti hiyo.

“Sote tunaweza kutoa mchango wetu wa kukabiliana na uzalishaji wa gesi chafu ardhini na kufikia malengo ya mwaka 2050,” amesema.

Ameongeza kuwa, matumizi ya sola yatauwezesha Msikiti huo kupunguza kwa kiwango kikubwa gharama za umeme na badala yake utaweza kushughulikia miradi mingine kama ya uzalishaji wa chakula na mengineyo. Msikiti huo mkuu wa Scotland una azma pia ya kuitisha vikao na mikutano mbalimbali ikiwemo ya kila mwaka kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii ya eneo hilo kuhusu hatari za uchafuzi wa tabianchi.

(Visited 13 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!