Mwandishi wa Qur’ani Tukufu mwenye umri mdogo zaidi nchini Misri amepewa kibali cha kuandika Kitabu hicho kitakatifu na Chama cha Waandishi wa Khat (Kaligrafia – Calligraphy) cha nchi hiyo.

Nilianza na walimu wasio na uzoefu lakini baada ya muda si mrefu nilifanikiwa kuwa na weledi mzuri katika uandishi, na nilikubaliwa kuwa mwalimu wa wanafunzi wapya katika chuo hicho hicho

Mtandao wa al Ahram umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Masad Khodair, maarufu kwa jina la Khudair al Porsaidi, Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Khat (Kaligrafia) cha Misri amemtunuku kibali Muhammad Marjan (19) mwandishi mwenye umri mdogo zaidi wa Khat nchini Misri cha kuandika Qur’ani Tukufu. Kijana huyo hivi sasa ni mwanachuo wa lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Bonde la Kusini (South Valley University) huko Qena, mashariki mwa Mto Nile.

Akielezea furaha yake isiyo na kifani, Muhammad Marjan amesema kuwa, kupata fakhari ya kuandika Qur’ani Tukufu kwa mkono wake na kwa Khat nzuri, ndiyo iliyokuwa ndoto yake tangu akiwa mtoto mdogo. Amesema si jambo rahisi kuweza kupata kibali hicho, kwani uandishi wa Qur’ani Tukufu una sheria ngumu sana zikiwemo Khat nzuri za kuvutia, kipaji na ubunifu katika uandishi.

Anasema, amejifunza fani ya Khat (kaligrafia) katika chuo maalumu cha kufundishia fani hiyo.

 “Nilianza na walimu wasio na uzoefu lakini baada ya muda si mrefu nilifanikiwa kuwa na weledi mzuri katika uandishi, na nilikubaliwa kuwa mwalimu wa wanafunzi wapya katika chuo hicho hicho,” amesema kijana Marjan.

Sasa hivi anasema, anawafundisha watu mbalimbali fani ya kaligrafia wakiwemo madaktari na wahandisi wa nyuga mbalimbali ambao wanaipenda fani hiyo.

(Visited 69 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!