1. Allah jina takatifu, naanza ya Rahmani
  Kwa jina Lako Latwifu, baraka za Ramadhani
  Samehe hai na wafu, sote tuwe neemani
  Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Turudi Kwake Raufu, Yaayyuha waumini
  Tusijifanye vipofu, kuasi wetu Manani
  Tujipange safusafu, kwa toba misikitini
  Rabbi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Allah Rabbi utuafu, tumezama madhambini
  Mja kiumbe dhaifu, hajali jema ni nini
  Hutesa hata siafu, amshinda hayawani
  Rabbi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Nyoyo zetu zi jafafu, ni kavu hatubaini
  Rutubaye ni hafifu, tarutubishwa na nini
  Kama si zako Arifu, kwa wajao samahani
  Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Tutende uadilifu, amri ya yetu dini
  Tusione takilifu, kurejea kwa Rabbani
  Nyoyo ziingie khofu, tujue tu masikini
  Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Mola wetu ni Latifu, twaasi tu madhambini
  Atusamehe Raufu, huruma nyingi pomoni
  Kumi hili takatifu, fursa tusitupeni
  Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

***

 1. Leo hai kesho mfu, zitajapita awani
  Bila ya Mola kukhofu, hakuna cha nusurani
  Toba kitu maalufu, tutubu dhambi jamani
  Rabi turuzuku toba, ni kumi la ghufurani.

Na Ahmed Rashid.

(Visited 9 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!