Mkuu wa jimbo la Niger (Niger State) la katikati mwa Nigeria na ambalo ndilo jimbo kubwa zaidi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ametangaza habari ya kufunguliwa kituo kikuu cha mafundisho ya Qur’ani katika jimbo hilo kwa ajili ya kudhibiti watoto wanaozurura mitaani.

Mtandao wa “Naija 247 News” umeripoti habari hiyo na kumnukuu mkuu wa jimbo hilo Malam Abubakar Bello akisema kuwa, amefungua kituo kikuu cha usomeshaji wa Qur’ani katika jimbo lake kwa lengo la ni kuhakikisha mpango wa kuhifadhi kwa pamoja Qur’ani Tukufu unalindwa katika ratiba za masomo ya Skuli za Msingi za jimbo hilo.

Amesema, kuanzisha kituo hicho kikuu cha usomeshaji wa Qur’ani ni sehemu ya mipango wa serikali ya kukabiliana na watoto wanaozurura mitaani na kwamba mbali na masomo ya kawaida shuleni, kuna ratiba maalumu za masomo ya Qur’ani Tukufu ili kutotoa fursa kwa watoto kuzurura na kufanya kazi barabarani.

Vile vile ameelezea kusikitishwa kwake na kuweko utitiri wa vituo vyenye dahalia za kuhifadhi watoto wadogo wenye umri wa baina ya miaka minane hadi 10 akisisitiza kuwa, kundi hilo la watoto liko hatarini kutumiwa vibaya kwa sura za kila namna  pamoja na kushinda na njaa na kukumbwa na maradhi chungu nzima. Amesema watoto hao wanakosa malezi ya baba na mama na hilo ndilo tatizo kubwa nchini Nigeria. Mkuu huyo wa jimbo la Niger nchini Nigeria vile vile ametoa amri kwa shule zote za msingi kuhakikisha kuwa masomo ya dini ya Kiislamu yanapewa nafasi kubwa katika ratiba zao za masomo ili kuwatunuku watoto maadili bora na kukabiliana vizuri na uhalifu na vitendo viovu.

(Visited 59 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!