Ofisi ya Biashara na Viwanda ya Abuja, mji mkuu wa Nigeria imetangaza mpango wa kuitishwa maonyesho ya kimataifa ya Bidhaa Halalikatika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kwa mujibu wa Pakistan Observer, ofisi hiyo ya kibiashara na viwanda ya Abuja (ACCI) imetangaza kuwa, lengo la maonyesho hayo ni kunyanyua uwezo wa jamii za Kiislamu ya nchi hiyo kupata bidhaa na huduma zinazolingana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Zaidi ya mashirika 70 ya bidhaa na sekta mbalimbali zikiwemo vyakula, vinywaji, bidhaa za mapambo, nguo, utalii wa kidini na mahoteli na mikahawa ya Kiislamu yamethibitisha kushiriki katika maonyesho hayo.

Wasomi na wataalamu zaidi ya 22 watazungumza kuhusu sekta na bidhaa halali kutoka nchi 10 tofauti, wakati wa maonyesho hayo.

Maonyesho hayo ya kimataifa ya bidhaa za halali yamepangwa kufanyika tarehe 14 hadi 16 Septemba 2021. Mashirika yaliyothibitisha kushiriki katika maonyesho hayo ni kutoka Nigeria, Uturuki, India, Malaysia, Indonesia, Misri, Tunisia, Morocco, Imarati (UAE) na Saudi Arabia.

Ikumbukwe kuwa, sekta ya Bidhaa za Halali inaingiza pato la dola trilioni 3 kwa mwaka na ni soko lenye uhakika mno katika uchumi wa dunia. Soko hilo ni la Waislamu bilioni 1.8, sawa na robo nzima ya watu wote duniani. Soko la Bidhaa Halali lina fursa nyingi za kukua na kustawi.

(Visited 93 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!