Bisimillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema ametuwekea njia nyingi sana za kuweza mtu kujiandalia mazingira mazuri ya kuendelea kupokea wimbi kubwa la thawabu hata baada ya kufariki dunia. Kuna suala la kusomesha elimu yenye manufaa na sadaka za kuendelea zinazojumuisha hata neno jema n.k. Lakini hapa sisi tumeamua kuorodhesha njia sita nyepesi kati ya nyingi sana za kuweza kupata neema hiyo hata baada ya kuondoka duniani. Lililo muhimu ni kufanya mambo haya kilillahi, kwa ikhlasi na kwa ajili tu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

1 – Mpe mtu mmoja Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani; kila atakapokuwa anasoma Qur’ani na yeyote atakayefaidishwa na Qur’ani hiyo kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, thawabu zake zitaendelea kukufikia popote ulipo hata Akhera. Muhimu ni ikhlasi.

2 – Peleka kigari cha wagonjwa hospitalini au sehemu ya kuhudumia wagonjwa. Mgonjwa yeyote atakayetumia kigari hicho thawabu zake zitakufikia popote ulipo. Muhimu ni ikhlasi.

3 – Shiriki katika ujenzi wa Msikiti hata kwa nguvu zako kama uwezo wa mali huna. Thawabu zake zitaendelea kukufikia popote ulipo maadamu eneo hilo ataendelea kuabudiwa Allah. Muhimu ni ikhlasi.

4 – Weka bomba la maji safi katika eneo lenye watu wengi ikiwezekana maji baridi sehemu zenye joto. Thawabu zake zitaendelea kukufikia popote ulipo kwa kila atakayekunywa maji hayo. Muhimu ni ikhlasi.

5 – Panda japo mti mmoja uufanye wakfu kwa watu. Yeyote atakayefaidika na kivuli na matunda yake, thawabu zake zitaendelea kukufikia popote ulipo hata baada ya kufariki dunia. Muhimu ni ikhlasi.

6 – Ambalo ni rahisi zaidi, wafikishie wengine ujumbe huu kadiri unavyoweza. Huenda kati ya hao akatokea japo mmoja akatekeleza moja ya haya mambo sita, ikawa ni sababu ya Mwenyezi Mungu kukumiminia thawabu popote ulipo hata baada ya kuondoka duniani. Muhimu ni ikhlasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!