Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetangaza kuwa inaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kurahisisha mazungumzo baina ya makundi hasimu nchini Sudan na kusisitiza kuwa, juhudi hizo ni muhimu kuendelea.

Tovuti ya al Watan imeripoti habari hiyo kwa kuinukuu sekretarieti ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema, inaunga mkono juhudi zote za kieneo na kimataifa za kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Sudan.

Jumuiya hiyo aidha imezitaka pande husika nchini Sudan kuyapa umuhimu zaidi maslahi ya taifa na ya wananchi, kujiepusha na fujo na mabavu na badala yake yafanya juhudi za kutafuta njia za amani za kuimarisha demokrasia, usalama, amani na ustawi wa nchi yao.

Katibu Mkuu wa OIC, Hussein Ibrahim Taha raia wa Chad amesema katika taarifa hiyo kwamba jumuiya hiyo itaendelea kuiunga mkono Sudan katika juhudi za kudhamini usalama, utulivu na umoja wa kitaifa pamoja na ustawi wake katika nyuga zote.

Amesema, OIC itatumia uwezo wake wote kuunga mkono mazungumzo baina ya makundi ya Sudan hasa wakati huu ambapo nchi hiyo inapitia kipindi kigumu cha mpito. Umoja wa Mataifa umesema kuwa, mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Sudan yalianza Januari 8, 2022 kwa shabaha ya kufikia makubaliano ya kudumu ya kukomesha mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!