*Asema, haikuwa rahisi

Na Bakari Mwakangwale

ULEMAVU wa Macho haukuwa kikwazo kwa  Bi. Aisha Salum, katika juhudi za kujiendeleza kielimu, na sasa anatimiza ndoto yake akiwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, akisoma Shahada ya juu (uzamili).

Haikuwa rahisi kwake kufikia hatua ya kupata Shahada ya kwanza na sasa ya pili, kutokana na mazingira aliyopitia ya kuitafuta elimu akiwa katika ulemavu wa macho huku akitoka katika familiya yenye hali duni.

Mahojiano na gazeti la Annur

Akiongea na Gazeti la Anuur, Bi. Aisha, alisema kwa sasa anasoma Shahada ya pili katika Sanaa ya Habari na Mawasiliano huku akisema amepambana kuweza kufika hapo kielimu huku akiwa katika hali hiyo toka akiwa Shule ya Msingi.

Bi. Aisha aliyezaliwa mwaka 1981, Mkoani Singida, akiwa ni mtoto wa 16, katika familia yao, anasema kutokuona kwake kulisababishwa na ugonjwa wa Surua aliopata akiwa mdogo na kumuathiri katika mboni ya macho na kusababisha kutokuona kabisa.

Nilizaliwa sina ulemavu wa macho lakini baada ya miaka sita nikapoteza hali ya kuona na kupata ulemavu wa macho, baada ya kuugua ugonjwa wa surua na kuniweka katika wakati mgumu wa kuweza kusoma kuanzia hapo. Amesema Bi. Aisha.

Hata hivyo alisema, alishauriwa kuwa anaweza kusoma katika hali hiyo ya ulemavu wa macho, hivyo akawashauri wazazi wake wampeleke shule wakaafiki na kumpeleka Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko iliyopo Ikungi, Mkoani Singida.

Masomo na changamoto 

Alisema, alianza kusoma mwaka 1990 na kuhitimu darasa la saba mwaka 1996, ambapo alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Kilosa, Mkoani Morogoro, na hapo ndipo alipoanza kukutana na changamoto ikiwemo suala la ada, kutokana na  wazazi wake kuwa na uwezo mdogo kiuchumi.

Alisema, hali hiyo ilisababisha kuchelewa kujiunga kidato cha kwanza, hali kama hiyo iliendelea pia akiwa kidato cha pili na alipofanikiwa kuingia kidato cha tatu, alipata mfadhili aliyemlipia ada yote.

Kidato cha nne, tatizo la ada lilijirudia na kusababisha nishindwe kusoma kwa ufasaha hivyo ilinilazimu kurudi kijijini nikiwa sijamaliza mitihani yangu na kuondosha matumaini ya kuendelea na masomo zaidi. Amesema Bi. Aisha.

Bi. Aisha alisema hamu ya kuendelea na masomo ilikuwa ikimsumbua kichwani, hata hivyo akasema akakata shauri na kuwaaga wazazi wake kuwa ana kwenda Dar es Salaam, kuna kazi ya kwenda kufanya.

Na kweli haikuwa rahisi

Hata hivyo alisema, haikuwa kazi rahisi kuweza kuruhusiwa kuondoka kwanza wakiamini hawezi kupata kazi kutokana na hali yake na hata kuweza kuendelea na masomo kutokana na uwezo wao wa kifedha kuwa mdogo.

“Niliwashawishi kisha waliniruhusu lakini lengo langu niondoke nikapambane ili niweze kupata elimu, nilifika Dar es Salaam, nikiwa sina mahali pakufikia kwa kuwa sikuwa na ndugu.”

Nilimuomba dereva wa basi anisaidie nifike Shule ya Msingi Uhuru, niliamini pale nitapata hifadhi, baada ya hapo nilipitapita kwa watu kuomba wanisaidie kunilipia ada ili niweza kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa kuwa nilisoma lakini sikumaliza. Amesema Bi. Aisha.

Penye nia pana njia

Alisema, alijiamini kuwa anaweza kufanya mtihani wa Taifa, wa kidato cha nne na alibahatika kumpata mtu aliyemlipia Kituo cha Mtihani mwaka 2008, katika Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim Jijini Dar es Salaam.

Alisema, alifanikiwa kujiandaa na kufanya Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne, na alipata matokeo yaliyomuwezesha kuendelea na Chuo, ngazi ya cheti ambapo mwaka 2010, alipata mtu aliyemdhamini kwa kumlipia ada na kujiunga Chuo cha Bagamoyo kwa ngazi ya Cheti na Diploma.

“Nilipoomba kujiunga katika Chuo cha Bagamoyo, walinikatalia waliniambia nitawezaje kusoma kozi hiyo nikiwa sioni wakaniambia hawana mwalimu wa kuweza kunisaidia.”

Niliwauliza kama wanafahamu maana ya Inclusive Education, niliwaambia sioni lakini akili inafanya kazi na masikio yanasikia, nikasimamia hoja yangu ya kuomba waniruhusu nisome, hatimae waliniruhusu ili waone kama nitaweza. Amesema.

Alisema, mwisho wa siku alihitimu masomo na kufanikiwa kufanya vizuri, kwani akasema kati ya wanafunzi 260, waliohitimu yeye alikuwa  mwanafunzi wa kwanza kwa kupata daraja la kwanza (First Class) na kutunikiwa zawadi, hali iliyowashangaza wengi.

Changamoto zaidi

Akizungumzia changamoto alizokumbana nazo katika kuyaendea masomo yake katika hali hiyo ya ulemavu wa macho, alisema akiwa Shule ya Msingi hali haikuwa mbaya, akasema matatizo yalikuja alipoanza Sekondari.

Alisema, mbali ya kukabiliwa na tatizo la ada, na kuchelewa kwenda Sekondari, baada ya kwenda Sekondari aliyopangiwa (Kilosa Sekondari) hakukuwa na kifaa maalum cha kusomea walemavu wa macho.

“Sekondari niyosoma ilikuwa mchanganyiko ila wasichana walemavu tulikuwa wanne darasani hapakuwa na taipreta, kila mmoja alifanya juhudi ya kupata kwa juhudi zake mimi niliazimiwa kutoka Sekondari ya Mzumbe Morogoro, hata hivyo ilikuwa mbovu. Amefafanua Bi. Aisha.  

Bi Aisha anaendelea kusimulia

Alisema, akiwa chuoni Bagamoyo alipata mashine maalum ya walemavu wa macho inayotoa maandishi ya nukta nundu, na walimu walikuwa wanamtafuta mfasiri na kuingiza katika maandishi ya kawaida.

Alisema, matokea aliyoyapa Chuo cha Bagamoyo, yalimpa nguvu kuendelea na elimu ya juu ambapo mwaka 2015, alijiunga Chuo Kikuu cha Tumaini, kusoma Digrii ya kwanza na alibahatika kupata Mkopo Serikalini.

Bi. Aisha, alisema alifanya vizuri Chuo Kikuu cha Tumaini na kutunukiwa Shahada ya kwanza, Mwaka 2019,  alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa ajili ya kusoma Digrii ya Pili (Shahada ya Uzamili) akiwa hana mtu yoyote wa kumlipia Ada, lakini hakukata tamaa akiamini atapambana kupata ada akiwa Chuoni.

Amtegemeaye Mungu, hamuachi mkono

Namshukuru Mungu, nilipata msamaria akanilipia sehemu ya Ada, hata hivyo baada ya hapo sikujua nielekee wapi tena kupata msaada wa kumalizia ada yangu.”

“Nilishauriwa kuwa niitafute Taasisi ya WIPAHS, kwani wao huwa wanasaidia katika masomo, nilituma maombi ya kusaidiwa, nilikubaliwa nao wakanilipia kiasi cha ada kilichobakia na sasa nimemaliza deni.” Amesema Bi. Aisha.

Kinachomuumiza zaidi

Bi. Aisha alisema huwa anaumia kusikia walemavu kama yeye kuwapo mitaani wakiomba na wengine wamemaliza kidato cha nne, lakini hawana mwamko wa kusema wapambane kujielimisha lakini wanaona kuomba kwao ndio imekuwa ajira.

Kwa upande mwingine, Bi. Aisha, amewashukuru wote walioweza kumsaidia kuanzia mtu mmoja mmoja, ikiwemo Taasisi ya Wipahs, akawaomba waendelee kumsaidia na kumshika mkono, kwani bado anakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa hisani ya Annur

 

(Visited 52 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!