Ibada za Kiislamu zinavyofanyika katika viunga vya mji wa Cape Town huko Afrika Kusini zimepunguza vitendo vya uhalifu mjini humo.

Mtandao wa About Islam umeripoti habari hiyo na kusisitiza kuwa, Waislamu wanaamini kwamba kumkumbuka Mwenyezi Mungu kunaleta utulivu katika maisha na jamii za wanadamu.

Huko katika mji wa Manenberg, kwenye viunga vya mji wa Cape Town, Afrika Kusini, ibada za Kiislamu zinazofanyika mjini humo zimesaidia sana kuleta utulivu na kupunguza uhalifu kwenye eneo hilo zima.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kundi moja la masheikh na mubalighina walichukua jukumu la kurejesha utulivu katika eneo hilo ambalo lilikuwa ni hatari kwa usalama wa raia. Magenge ya wahalifu, majambazi na madawa ya kulevya yalikuwa yametamalaki katika eneo hilo.

Walichofanya mubalighina na masheikh hao mbali na ibada nyinginezo; ni dhikr na kumtaja Mwenyezi Mwenyezi Mungu na sifa zake kwa sauti nzuri wiki mara moja kwenye sehemu ya wazi katika eneo hilo.

Wanaoendesha kampeni hiyo wanasema, katika kipindi chote hiki cha miaka mitatu, hakuna tukio lolote la uhalifu au shambulio au ujambazi lililotokea katika kipindi cha saa moja na nusu ya ibada kwenye eneo la wazi ambalo hushirikisha watu baina ya 100 hadi 400.

Sheikh Mogamad Saalieg Isaacs ambaye ndiye anayeongoza kampeni hiyo, ameliambia shirika la utangazaji la BBC kwamba cha kufurahisha ni kuona kuwa wameweza kuendeleza ibada hizo katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo licha ya kukumbwa na changamoto nyingi.

Mwaka 2015 jeshi la polisi la Afrika Kusini liliutangaza mji wa Manenberg kuwa ni eneo hatari sana. Rangi ya mji huo kwa mujibu wa jeshi hilo la polisi, ilikuwa nyekundu. Hali ilikuwa ni mbaya kiasi kwamba kwa muda wa miezi mingi, magari ya wagonjwa yalikuwa hayathubutu kuingia kwenye mji huo bila ya ulinzi wa polisi.

Hata hivyo, vikao, ibada za Waislamu zimebadilisha hali ya mambo, uhalifu umepungua na Waislamu wametunukiwa nishani ya ushujaa na polisi wa mji huo. Sheikh Isaacs anasema, kusoma kwao majina ya Mwenyezi Mungu katika eneo la wazi kwa sauti kubwa na kwa sauti nzuri, kumeleta utulivu katika nyoyo za wakazi wa mji huo na kupunguza vitendo vya uhalifu.

Amesema, zoezi hilo hufanyika wiki mara moja. Kama tungeliweza, tungefanya ibada hizo kila siku kwani taathira zake ni kubwa sana. Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha utafiti cha Pew ya mwaka 2010, idadi ya Waislamu Afrika Kusini ni asilimia 1.5 ya wakazi wote karibu milioni 59 wa nchi hiyo. Dini tukufu ya Kiislamu ndiyo inayoenea kwa kasi zaidi kuliko dini zote huko Afrika Kusini. Waafrika Kusini asili ndio wanaoingia zaidi katika dini ya Kiislamu. Ripoti hiyo inaendelea kusema, kati ya mwaka 1991 hadi 2004 idadi ya Waislamu nchini Afrika Kusini iliongezeka mara sita nchini Afrika Kusini.

Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za ibada hizo.

(Visited 27 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!