Bi Shatita Abdul ‘Azīm Darwish (ستیته عبدالعظیم دوریش), ni bimkubwa wa miaka 58 raia wa Misri ambaye umri wake wote ameuweka wakfu kwa ajili ya kukitumikia Kitabu cha Allah cha Qur’ani Tukufu. Bi Shatita amehifadhi Qur’ani nzima.

Bi Shatita Abdul ‘Azīm Darwish (ستیته عبدالعظیم دوریش), ni bimkubwa wa miaka 58 raia wa Misri ambaye umri wake wote ameuweka wakfu kwa ajili ya kukitumikia Kitabu cha Allah cha Qur’ani Tukufu. Bi Shatita amehifadhi Qur’ani nzima.

Mtandao wa habari wa al Yaum al Saabi’i umemnukuu Bi Shatita akisema: Nimezaliwa katika kijiji cha al Ramla katika mji wa Belbes wa mkoa wa al Sharqiya nchini Misri, nikiwa na matatizo ya kutoona vizuri. Nimefanyiwa oparesheni nyingi za macho lakini hali yangu haikutengamaa. Nilikuwa ashiki na mpenzi mkubwa wa kusikiliza qiraa ya Qur’ani Tukufu ya baba yangu ambaye alikuwa ni Imam na mtoaji mawaidha Msikitini. Ndio maana nilipotimia miaka minne nilijiunga na chuo cha Qur’ani katika kijiji chetu kwa Sheikh Abdul Rahman AwadhuLlah na nikaanza kujifunza Qur’ani wakati huo.

Alihifadhi Qur’ani nzima akiwa mdogo

Bi Shatita anaendelea kusimulia maisha yake akisema: Nikiwa na umri wa miaka 9 nilikuwa tayari nimeshahifadhi Qur’ani nzima. Kutokana na kipaji changu, Sheikh Abdul Rahman aliniamini na kunipa jukumu la kusimamia kazi ya kuwahifadhisha Qur’ani wanafunzi wenzangu darasani mwetu ambao walikuwa dhaifu. Zama hizo tulikuwa tukiandika Qur’ani kwenye loho za mbao. Mimi umri wangu wote nimeusabilia katika kusoma na kuhifadhi na kusomesha na kuhifadhisha Qur’ani Tukufu. Nilikuwa nikiitwa kusoma Qur’ani wakati watu walipokuwa wanafariki dunia na nilikuwa maarufu kwa jina la qarii mwanamke.

Maisha yake ya ndoa na familia

Akiendelea kuelezea maisha yake, bimkubwa huyu ambaye umri wake wote ameutoa wakfu kwa ajili ya kuitumikia Qur’ani Tukufu anasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu alinitunuku mume mwema. Mke wake wa kwanza alikuwa amefariki dunia na alikuwa na watoto watano wa rika tofauti. Juhudi zetu zote tulizielekeza kwenye kuwalea watoto hao na mimi ninawaona kama niliowazaa mwenyewe na nimewalea mpaka walipofanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali. Mtoto mkubwa amekuwa mkuu wa shule. Mtoto anayefuata ni mtu wa viwanda. Mtoto wa tatu ni mhadhiri wa chuo kikuu. Wa nne ni mtu wa kutengeneza dawa na wa tano ambaye ni wa kike bado anaendelea na masomo.

“Hata baada ya kufariki dunia mume wangu, wenetu hawa wako pamoja nami muda wote kwa shida na raha. Kwa kweli nimebahatika sana, Alhamdulillah.”

Nimepata bahati ya kupata mume mwema na watoto wema na kwa kweli watoto wa mume wangu ni watu wazuri sana. Hata baada ya kufariki dunia mume wangu, wenetu hawa wako pamoja nami muda wote kwa shida na raha. Kwa kweli nimebahatika sana, Alhamdulillah. Anasema, katika ndoa yake hiyo amejaaliwa kupata watoto wawili wa kike na kuongeza kuwa, Faatimah amemaliza masomo ya malezi ya watoto na Asma amemaliza masomo ya fasihi ya lugha ya Kifaransa. Watoto wa mume wangu na wanangu wawili niliowazaa wananipenda na wanapendana sana na huwezi kujua kuwa ni wa mama tofauti.

Matatizo yake ya macho

Alipoombwa na mwandishi wa al Yaum al Saabi’I aseme machache kuhusu matatizo yake ya kutoona vizuri, hafidha huyo wa Qur’ani nzima amesema: Ilikuwa imebakia kidogo tu nipoteze kikamilifu nuru ya macho kwani matatizo yangu ya kutoona vizuri yalikuwa yanazidi kuwa makubwa kadiri umri wangu ulivyokuwa mkubwa. Pamoja na hayo niliendelea na kazi zangu kama kawaida za kulea na kushughulikia familia yangu. Qur’ani imetia baraka nyingi ndani ya nyumba yangu na ni kheri ambayo kamwe haijawahi kukatika ndani ya familia yangu.

Mafanikio katika kazi ya Qur’ani

Amma kuhusu shughuli zake nyingine, Bi Shatita anasema: Ninaanza siku yangu kila siku kwa Sala na kusoma Qur’ani Tukufu. Shughuli zangu nyingine ni kwenda katika kituo cha kutoa mafunzo mbalimbali, hata hivyo kwa vile hivi sasa skuli zimefungwa, nimeamua kuwahamasisha wanafunzi waje nyumbani kwangu kwa ajili ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Ninafanya kazi hiyo kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu tu na hakuna malipo yoyote wanayotoa wanafunzi hao. Amma kuhusu mafanikio yake katika suala hili la kuyafanya maisha yake yote kuwa wakfu wa kuitumikia Qur’ani Tukufu, Bi Shatita anasema: Katika muda huu wa nusu karne wa kuitumikia Qur’ani Tukufu, amepata taufiki ya kusomesha wanafunzi wengi Qur’ani Tukufu ambao hivi sasa wana nyadhifa mbalimbali kama vile madaktari, wahandisi, maimamu misikitini, walimu n.k. Anasema katika kijiji chetu huwezi kupata nyumba yoyote ila watoto wa nyumba hiyo wamepitia kwetu kujifunza Qur’ani Tukufu.

Nasaha zake

Alipoulizwa kuhusu nasaha zake kwa watu wa familia amesema: Ninazishauri familia zote ziwalee watoto wao tangu wadogo katika malezi ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Wawapeleke watoto wao katika vituo vya kuhifadhi Qur’ani wakiwa bado wadogo kwani Qur’ani ina Baraka nyingi za duniani na Akhera kwa kila mtu. Baadaye amenukuu Hadithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW akisema: Yeyote anayetaka mafanikio ya duniani, basi ajifunze na ashikamane na Qur’ani na yeyote anayetaka maisha bora ya Akhera basi ajifunze na ashikamane na Qur’ani na yeyote anayetaka yote hayo mawili, basi pia ajifunze na ashikamane na Qur’ani Tukufu.

Hapa chini tumeweka baadhi ya picha zake

(Visited 20 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!