Omar Makki, mtoto wa miaka 6 raia wa Misri aliyehifadhi Qur’ani nzima, amefanikiwa kuwa mwanachama mwenye umri mdogo zaidi wa Chama cha Maqarii na Mahufadh (wasomaji na waliohifadhi) wa Qur’ani Tukufu nchini Misri. Qarii Makki, anatoka mkoa wa Sharqia wa kaskazini mwa Misri.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi’i, mtoto huyo wa miaka 6 amefanikiwa kuwa mwanachama cha Chama cha Maqarii na Mahufadh wa Qur’ani Tukufu nchini Misri na hivi sasa amekuwa balozi wa chama hicho wa kuwaelimisha  watu kuhusu ugonjwa wa COVID-19 na njia za kukabiliana na ugonjwa huo.

Nuru ya Qur’ani inaonekana muda wote katika kipaji cha sura yake ya kimaasumu. Muda wote anaonekana na bashasha, na watu wote – wakubwa kwa mdogo – wanampenda. Katika kampeni yake, mtoto Omar anawasomea watu Qur’ani tukufu kabla ya kuwahamasisha kuchunga protokali za kiafya za kujiepusha na ugonjwa wa COVID-19. Anawasomea pia hadith na mafundisho ya Uislamu ya wajibu wa kutunza usafi muda wote.

Miezi minne iliyopita, hafidhul Qur’an, Omar na ndugu yake wa kike, Nur, mwenye umri wa miaka mine, walitunzwa nishani na kupewa zawadi na Dk Mamdouh Ghorab, mkuu wa mkoa wa Sharqia kwa jitihada zao za kuhifadhi Qur’ani Tukufu na kuwasaidia wanakijiji wenzao.

Omar ni mtoto mdogo zaidi wa familia ya Misri ambaye mbali na kuwa mwanachama wa Chama cha Maqarii na Mahufadh wa Qur’ani Tukufu mkoani Sharqia, vile vile ni mjumbe mwenye umri mdogo zaidi wa Baraza la Uongozi la Umoja wa Mabaraza ya Wananchi wa Misri. Vile vile ni mshauri wa masuala ya watoto wadogo katika Baraza la Taifa na la Afrika la Haki za Binadamu la Misri.

Kwa mujibu wa mtandao huo wa al Yaum al Sabi’i mtoto Omar aidha ni msemaji wa watoto wa Misri katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na vile vile ni balozi wa watoto wadogo wa Baraza la Ulama na Wavumbuzi wa Misri na Ulimwengu wa Kiarabu.

Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za mtoto huyo, akiwa katika harakati zake na jinsi watu mbalimbali wanavyompokea kwa shauku na mapenzi makubwa.

(Visited 87 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!