Msikiti wa Nizamiye unaojulikana kwa majina maarufu ya Nizamiye Mosque na Nizamiye Masjid, ndio Msikiti mkubwa zaidi katika eneo la nusu ya kusini ya dunia. Msikiti huo uko katika mji wa Midrand wa Manispaa ya Johannesburg, Afrika Kusini.

Ramani na mchoro wa Msikiti huo uliandaliwa nchini Uturuki lakini ulijengwa na mhandisi majengo wa Afrika Kusini. Ujenzi wa Msikiti huo ulianza mwezi Oktoba 2009 na kumalizika mwaka 2012.

Msikiti huo umejengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 10. Hata hivyo majengo yenyewe yametumia ardhi isiyofikia hekta 7. Ramani na mchoro wa Msikiti huo umebuniwa na Ali Katırcıoğlu, mfanyabiashara wa Uturuki. Na umejengwa kwa mtindo wa usanifu majengo wa Ufalme wa Uthmania (Ottoman Empire). Ali Katırcıoğlu aliamua kujenga Msikiti huo nchini Afrika Kusini baada ya kukosa sehemu nzuri nchini Marekani. Hatimaye mhandishi majengo wa Afrika Kusini alianza kazi ya ujenzi mwaka 2009 na mwezi Oktoba 2012, ujenzi ulimalizika. Msikiti huo ulifunguliwa na Jacob Zuma, rais wa wakati huo wa Afrika Kusini.

Jina la Msikiti huo linarejea katika karne ya 11 Hijria, enzi za kushamiri madrasa, skuli na vyuo vya kidini vya Nidhamiyya, mjini Baghdad Iraq. Huo ulikuwa ni wakati wa utawala wa Abu Ali Hasan ibn Ali Tusi (aliyeishi baina ya Aprili 10, 1018 hadi Oktoba 14, 1092). Akijulikana kwa jina maarufu la Nizam al Mulk huko Iraq.

Nizamiye ni mjumuiko wa majengo kadhaa kama Msikiti, skuli, zahanati, soko na sehemu ya kuzikia Waislamu. Msikiti huo una kuba kubwa lenye uzito wa tani 47 ambalo limejengwa kwa risasi. Pembeni mwa kuba hilo, kuna makuba mengine manne ya ukubwa sawa na makuba mengine 21 madogo madogo. Ndani yake Msikiti huo umenakishiwa vigae vya asili ya Uturuki.

Dari na kuta za Msikiti huo zimepambwa kwa maandishi ya Kiarabu. Eneo lake la kusalia lina uwezo wa kuchukua watu elfu 6 kwa wakati mmoja. Nje ya kumbi za nje ya Msikiti kumewekwa maeneo matano ya kutilia udhu. Kuba kuu la Msikiti huo hung’ara kwa rangi za kijani na hudhurungi katika siku za sherehe na minasaba mbalimbali.

Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za Msikiti huo.

(Visited 33 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!