Polisi katika mji mkuu wa Ufaransa Paris wamekwamisha masomo maalumu ya watoto yaliyokuwa yanaendeshwa katika Msikiti wa Omar bnil Khattab na kupelekea kufungwa kikamilifu masomo hayo.
Toleo la mtandaoni la jarida la al Mujtam’a limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, polisi wa Ufaransa kwa kushirikiana na maafisa wa wizara tofauti za nchi hiyo, wamefunga masomo maalumu ya lugha ya Kiarabu na Kiislamu waliyokuwa wanapewa watoto katika Msikiti wa Omar bnil Khattab mjini Paris.
Hammadi al Hamami, mmoja wa viongozi wa masuala ya Misikiti mjini Paris amesema, masomo hayo yalikuwa yakitolewa Jumamosi na Jumapili kila wiki kwa ajili ya watoto wa Kiislamu, lakini polisi wamefunga masomo hayo.
Itakumbukwa kuwa, mapema mwaka huu, wabunge wa Ufaransa walipasisha muswada uliolalamikiwa sana na ambao uliwasilishwa bungeni na serikali ya Emmanuel Macron kwa madai ya eti kukabiliana na wanaotaka kujitenga.
Tarehe 30 mwezi huu wa Machi 2021, wabunge wa Ufaransa wanatarajiwa kuupasisha rasmi muswada huo na kuufanya sheria kwa madai ya kutia nguvu misingi ya mfumo wa jamhuri.
Muswada huo unalenga kukandamia harakati za kidini kwa madai ya kuzuia uchochezi na kuenezwa fitna katika mitandao ya kijamii na pia kuzuia makundi ya kidini ya Ufaransa kupokea misaada kutoka nje ya nchi hiyo.