Hapa chini ndugu zangu wapenzi tumeweka kipande cha video cha usomaji tajwidi na qiraa ya ya marhum Sheikh Shahat Muhammad Anwar na mwanawe, Mahmoud Shahat video ambayo imeenea kwenye mitandao ya kijamii.

Sheikh Shahat Muhammad Anwar ni katika maqarii maarufu na wakubwa wa Misri. Alizaliwa tarehe 1 Julai 1950 na kufariki dunia tarehe 12 Januari 2008. Alizaliwa katika kijiji cha Kufr al Qazir katika mkoa wa Dakahlia wa kaskazini mashariki mwa Cairo, mji mkuu wa Misri.

Baada ya kufariki dunia baba yake, Sheikh Shahat alikwenda yeye na mama yake nyumbani kwa babu mzaa mama na kuishi huko na wajomba zake. Mmoja wa wajomba zake alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Hulmi Muhammad Mustafa, mmoja wa maqarii wakubwa wa tajwidi na hilo lilimvutia sana Sheikh Shahat Muhammad Anwar na kumfanya atie hima ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Alipata taufiki ya kuhifadhi Qur’ani nzima akiwa na umri wa miaka minane tu.

Hivi sasa Mahmoud Shahat Muhammad Anwar, mwana wa kiume wa Sheikh Shahat naye amefuata nyayo za baba yake na ni kijana wa miaka 35 ambaye ni maarufu sana katika ulimwengu wa Kiislamu sasa hivi kwa usomaji wa kuvutia wa Qur’ani Tukufu. Sheikh Mahmoud Shahat naye alionesha mapenzi ya Qur’ani akiwa bado mdogo suala ambalo lilimfurahisha sana baba yake na akaamua kumsaidia na kumshajiisha kwa kila hali mwanawe huyo.

Kipande hiki cha video hapa chini ni sehemu ya qiraa ya mtu na mwanawe ya aya za 31, 32 na 33 za Sura ya an Naaziat na hivi ndivyo wazazi wanavyotakiwa kulea vyema watoto wao ili wakiondoka duniani, watoto wawe ni kigezo cha fakhari kwa wazazi wao mbele ya Mwenyezi Mungu na waja Wake.

(Visited 29 times, 1 visits today)
2 thoughts on “Qiraa ya Qur’ani Tukufu ya Sheikh Shahat na mwanawe”
  1. MaashAllah.Ni bahati sana kupata wana kama hawa.Allah Atawahifadhi na kumlipa mzee aliyeitimikia dini kwa kusoma Kitabu cha Allah kwani kuna baadhi badala ya kurithi mambo ya khairati wengine wanariti uimbaji manyimbo.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!