Siku kadhaa sasa nilitaka nipate nafasi ya kuorodhesha miujiza yote ya Nabii Musa AS iliyotajwa ndani ya Qur’ani na niorodheshe pia ile miujiza tisa iliyosisitizwa kwenye hii sura ya al Israa n.k, lakini sijapata nafasi.

QURAN TUKUFU

Aya ya Leo…

Al-Isra’ 17:106

(وَقُرۡءَانࣰا فَرَقۡنَـٰهُ لِتَقۡرَأَهُۥ عَلَى ٱلنَّاسِ عَلَىٰ مُكۡثࣲ وَنَزَّلۡنَـٰهُ تَنزِیلࣰا)

Na Qur’ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.

??????????

Bismillahir Rahmanir Rahim.
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Siku kadhaa sasa nilitaka nipate nafasi ya kuorodhesha miujiza yote ya Nabii Musa AS iliyotajwa ndani ya Qur’ani na niorodheshe pia ile miujiza tisa iliyosisitizwa kwenye hii sura ya al Israa n.k, lakini sijapata nafasi.

Wakati napitia aya hii ya 106 ya Sura ya al Israa, limekuja swali kwa nini Qur’ani haikuteremshwa mara moja na mkupuo mmoja hapa duniani?

Kwa wenye fikra finyu wanaweza hadi leo kudhani hilo ni kosa na ni mapungufu ya kwa nini Qur’ani hawakuteremshiwa viumbe wa ardhini “jumlatan waahidatan,” kwa mkupuo mmoja.

Ukosoaji huo lakini ni wa watu ambao akili zao si timamu. Ni ukosoaji wa makafiri. Ni ukosoaji wa washirikina. Na ni ukosoaji wa watu wa motoni. Maana ukituliza akili kiduchu tu utaona kwamba ilikuwa ni dharura Qur’ani iteremshwe polepole na mafungu mafungu.

Hapa nitataja sababu nne kama zilivyosemwa na wenye ilmu. Sisi maamuma letu kubwa ni kunukuu tu.

Sababu ya kwanza.

Ijapokuwa Qur’ani kimeitwa ni Kitabu, lakini ni tilkal kitaab ni kitabu “kile kulee” si kitabu cha wanadamu ni cha Muumba Mjuzi wa kila kitu, na ndio maana kinatangaza mapema kabisa kwamba mimi si Kitabu mnachokijua, mimi ni Kitabu chenye uhakika, sina shaka ndani yangu, nyote mkikusanyika hamwezi kuandika hata sura fupi kabisa kama yangu. Mimi sitokani na fikra za watu kwamba wakae wafikiri wanataka kuandika nini, wawape watu wa kuhariri na kurekebisha hapa na pale. Hapana, mimi si Kitabu chepesi hivyo, sichukuliki kwa mkupuo mmoja.

Qur’ani ni Kitabu kitakatifu kilichoendana na matukio ya miaka 23 ya kuteremshwa kwake. Kama ilibidi kiendane na matukio ya miaka 23, ingewezekana kweli kushuka kwa mkupuo mmoja?

Kama Qur’ani ingezengumzia matukio ya Madina kwa mfano hata kabla Mtume hajahamia Madina, ingeingia akilini kweli? Hivyo mtu ukituliza akili kidigi tu, utajua kwamba ilikuwa ni dharura Qur’ani kuteremshwa kihibi kihibi.
Hiyo ni sababu ya kwanza.

Sababu ya pili ya kuteremshwa Qur’ani polepole

Qur’ani ni Kitabu kitakatifu kilichokusanya mambo yote. Ni Kitabu cha kuelimisha na wakati huo huo ni Kitabu cha utekelezaji wa mafundisho yake.

Utekelezaji wa mafundisho yoyote unataka muda. Hauwezi kufanywa kwa ghafla moja. Huwezi kumchukua mtoto wa darasa la kwanza ukammiminia elimu zote mpaka za chuo kikuu kwa mkupuo mmoja.

Jamii ya Waarabu na wanadamu wakati alipotumwa Mtume wa mwisho ilikuwa imeghariki kwenye maasi na ufisadi kutoka unyayoni hadi utosini. Ilitaka busara na hikma ya hali ya juu mno kuirekebisha.
Yalitakikana mapinduzi makubwa na yasingeliweza kufanywa ila na mja mtukufu mwenye sifa za Mtume Muhammad SAW aliyekamilika katika ubinaadamu wake.

Mapinduzi makubwa kama hayo hayawezekani kwa mkupuo mmoja. Hivyo lilikuwa ni jambo la dharura Qur’ani wateremshiwe viumbe duniani hatua kwa hatua kulingana na hali na mazingira na matukio ya zama husika.

Sababu ya Tatu
Amma sababu ya tatu kama wanavyotueleza maulamaa ni kwamba, Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye ndiye Kiongozi wa mapinduzi makubwa yaliyoletwa na Uislamu, ilikuwa ni wepesi zaidi kwake kupokea amri na mafundisho kidogo kidogo kutoka kwa Allah kwa ajili ya viumbe.
Naam, kwa ukamilifu wake wa kibinadamu, yaani kwa kuwa kwake mwanadamu kamili aliyetimiza sifa zote alizopangiwa na Muumba wake, Mtume Muhammad SAW alikuwa na uwezo wa kupokea amri zote kwa mkupuo mmoja na kuwafundisha wanadamu na majini kiukamilifu, lakini Allah alishamwambia Mtume Wake kwa jina lake la Taha kwamba hakuteremshiwa Qur’ani ili aingie mashakani. Hiyo ni sababu ya tatu.

Sababu ya Nne ni kwamba, Qur’ani iliteremshwa polepole na kwa mafungu ili kudumisha mawasiliano baina ya Mtume SAW na chemchemu ya wahyi. Lau kama Qur’ani yote ingeteremshwa kwa mkupuo mmoja, mawasiliano hayo yangekatika na yasingedumu kwa muda wa miaka 23.

Ndio maana aya ya 32 ya Sura ya 25 ya al Furqan ikawajibu makafiri kwa kuwaambia: Na wakasema waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur’ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

Aya hii ya 32 ya sura ya 25 ya al Furqan inaashiria sababu ya tatu ya kuteremshwa mafungu mafungu Qur’ani Tukufu, wakati hii aya tunayoizungumzia hapa ya 106 ya al Israa inaashiria sababu ya pili kama tulivyoona.

Naam, hakuna kitu ndani ya Qur’ani na katika Uislamu ila kina falsafa na hikma nyingi, lakini kwa wanaoondoa kufuli kwenye nyoyo zao na kutumia vyema akili zao.

Mapungufu yote yaliyomo kwenye maelezo haya nayabeba mwenyewe,
hakiri wa Allah, Ahmed Rashid.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

(Visited 28 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!