Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, itaukarabati Msikiti wa Najjashi wa kaskazini mwa nchi hiyo ambao ni moja ya Misikiti ya kale zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu. Msikiti huo uliharibiwa wakati jeshi la Ethiopia lilipokuwa linapigana na kundi la Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Msikiti wa Najjashi ambalo ni jina la Mfalme mwadilifu wa Habasha, kulikofanyika Hijra ya kwanza kabisa ya Waislamu wa mwanzoni mwa Uislamu kwa amri ya Bwana Mtume Muhammad SAW, uko umbali wa kilomita 790 kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Taarifa zinasema kuwa, wapiganaji wa Tigray waliushambulia kwa silaha nzito Msikiti wa Najjashi na kuharibu maeneo yake kadhaa ikiwemo minara yake.

Masahaba wa Mtume Muhammad SAW walipokewa vizuri sana na Mfalme Najjashi na wakapewa hifadhi nchini humo baada ya kukimbia mateso yasiyovumilika waliyokuwa wakipewa na washirikina wa Makkah.

Msikiti huo umejengwa katika eneo kubwa na pembeni yake kuna makaburi 15 ya Masahaba wa Mtume Muhammad SAW waliofika Habasha (Ethiopia ya hivi sasa) na kufanya tablighi ya Uislamu hata kabla ya Uislamu kufika mjini Madina, huko Hijaz, (Saudi Arabia ya hivi sasa).

Msikiti wa Najjashi ni kumbukumbu kubwa na ya kipekee ya Hijra ya kwanza kabisa ya Waislamu waliokimbia mateso ya Makureish wa Makkah.

Msikiti wa Najjashi ambao una hadhi kubwa sana mbele ya Waislamu wote duniani huku Waislamu wa Ethiopia wakiuita Msikiti huo kwa jina la Makkah ya Pili, uliharibiwa wakati wa mapigano ya mwezi Novemba 2020. Taarifa zinasema kuwa, wapiganaji wa Tigray waliushambulia kwa silaha nzito Msikiti huo na kuharibu maeneo yake kadhaa ikiwemo minara yake.

Naibu wa Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Kuhifadhi Mirathi ya Utamaduni ya Ethiopia ameiambia televisheni ya serikali ya nchi hiyo kwamba, kumeundwa timu maalumu ya wataalamu kwa gharama ya serikali ya nchi hiyo ili kutathmini hasara ulizopata Msikiti huo na kuanza mara moja kuukarabati.

(Visited 97 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!