Serikali ya Morocco, nchi ambayo ndiye mzalishaji mkubwa wa bangi duniani, jana ilipasisha muswada wa kuhalalisha ukulima wa bangi nchi hiyo kwa madumizi ya tiba. Muswada huo unasubiri kupasishwa na Bunge ili uwe sheria.

Sheria hiyo mpya inapendekeza kuundwa shirika la taifa la kusimamia na kuendesha sekta ya ukulima wa bangi. Pia inapendekeza kuundwa vyama vya ushirika vya kusimamia vizuri ukulima wa mmea huo wa madawa ya kulevya.

Hatua hiyo itatoa uhalali wa ukulima wa bangi uliokuwa umepigwa marufuku nchini humo na kuna uwezekano sasa uzalishaji wa madawa hayo ya kulevya ukaongezeka sana nchini humo. Serikali ya Morocco inasema, hatua yake hiyo ya kuhalalisha matumizi ya bangi katika matibabu itaogeza nafasi za ajira.

Mwanzoni mwa mwezi Disemba 2020, Tume ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na kudhibiti mihadarati ilipiga kura na kupasisha matumizi ya bangi kwa ajili ya matibabu.

Upigaji kura huo ulifanyika baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kupendekeza kuondolewa bangi katika orodha ya kundi la dawa hatari zaidi za kulevya. Hatua ya Umoja wa Mataifa ya kupasisha pendekezo hilo la WHO, imechochea uzalishaji wa bangi kwa matumizi ya kimatibabu.

Kati ya nchi 53 wanachama, 27 zilipiga kura ya kuunga mkono mapendekezo hayo WHO na nchi 25 zilipinga. Ukraine ilikuwa nchi pekee ambayo haikupiga kura.  Miongoni mwa mataifa yaliyopiga kura ya kuunga mkono mapendekezo hayo, ni Marekani na nchi za Ulaya huku China, Misri, Nigeria, Pakistan na Russia zikiwa miongoni mwa nchi zilizopinga kuhalalisha matumizi ya mmea huo.

Inakadiriwa kuwa, uzalishaji wa bangi nchini Morocco ulifika tani 700 mwaka 2020. Watumiaji wakubwa wa madawa hayo ya kulevya ni nchi za Ulaya. Morocco iko karibu sana na bara Ulaya, hivyo imekuwa kitovu cha uzalishaji wa mihadarati hiyo.

Mamlaka za Morocco zimetoa takwimu wiki hii na kusema kuwa, hekta 55,000 (karibu eka 136,000) za ardhi ya milima ya Rif ya kaskazini mwa nchi hiyo ilitumiwa kulima mmea wa bangi kinyume cha sheria mwaka 2019.

(Visited 111 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!