Mpya Kabisa

Shaykha Maryam, mwasisi wa kituo kikubwa zaidi cha Qur’ani Tukufu nchini Senegal

Shaykha Maryam Niasse maarufu kwa jina la Shaykha Maryam, ni mmoja wa watu muhimu sana walioitumikia Qur’ani katika umri wao wote nchini Senegal.

Kwa mujibu wa “Sahara Medias,” Shaykha Maryam ni maarufu sana nchini Senegal na katika nchi za magharabi mwa Afrika zinazopakana na nchi hiyo kutokana na kazi kubwa ya kusomesha Qur’ani ambapo umri wake wote aliuweka wakfu kwa ajili ya kazi hiyo ya kheri.

Shaykha Maryam akiendelea kufundisha Qur’ani hadi akiwa na umri mkubwa

Chuo chake cha Qur’ani

Chuo kikubwa zaidi cha Qur’ani Tukufu nchini Senegal kimeanzishwa na yeye. Chuo hicho kina matawi mengi ndani na nje ya Senegal. Maelfu ya wanafunzi wa nchi nyingi za magharibi mwa Afrika wamepata masomo yao ya Qur’ani Tukufu katika chuo cha Shaykha Maryam.

Bi Mwalimu huyo amepewa lakabu mbalimbali kama vile “Hadimu wa Qur’ani” na “Sayyida.”

Shaykha Maryam alizaliwa mwaka 1934 Milaadia katikati mwa mji mkuu wa Senegal, Dakar. Alizaliwa na kukulia katika familia ya Kisufi. Baba yake, Sheikh Ibrahim Niasse alikuwa mkuu wa Masufi wa Tijani, tariqa ambayo ni maarufu sana magharibi mwa Afrika.

Shaykha Maryam alizaliwa na kukulia katika nyumba ambayo muda wote ilikuwa inasomwa Qur’ani Tukufu. Alifanikiwa kuhifadhi Msahafu mzima akiwa bado mtoto mdogo. Alikuwa pia anazungumza lugha ya Kiarabu na alisoma pia fiqh na sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Shaykha Maryam

Mwaka 1984, Shaykha Maryam aliasisi Jumuiya ya Masomo ya Sheikh al Islam Alhaj Ibrahim Niasse na makao makuu yake ni Dakar, mji mkuu wa Senegal. Taasisi hiyo ni moja ya vituo vikuu vya kusomesha Qur’ani na mafundisho ya dini ya Kiislamu nchini Senegal na eneo zima la magharibi mwa Afrika.

Shaykha Maryam alifariki dunia Jumamosi iliyopita, tarehe 26 Disemba 2020 akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuupitishia muda wake wote kufundisha Qur’ani Tukufu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!