Misikiti ya miji kadhaa ya Ujerumani imeamua kufanya sherehe za “Milango Wazi ya Misikiti” kama sehemu ya kusherehekea siku Ujerumani Magharibi na Ujerumani Mashariki zilipoungana.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa “IM EXPACT” ambao umeongeza kuwa, misikiti ya miji kadhaa nchini Ujerumani imeamua kuweka milango yake wazi tarehe 3 Oktoba mwaka huu kama sehemu ya sherehe za kuungana Ujerumani Magharibi na Ujerumani Mashariki  ili watu wa dini na itikadi tofauti waweze kuingia kwenye misikiti hiyo, tab’an kwa kuchunga sheria za Kiislamu na kama watakuwa na maswali yoyote kuhusu Uislamu waweze kuuliza.

Si hayo tu, lakini Waislamu wa Ujerumani wameamua kutumia fursa hiyo kutangaza mafundisho sahihi ya Uislamu, utamaduni wa Kiislamu, vyakula vya Waislamu na maonyesho mengine mbalimbali.

Sherehe hizo zinafanyika kwa usimamizi wa Baraza Kuu la Waislamu wa Ujerumani. Zaidi ya misikiti elfu moja ya Ujerumani itashiriki kwenye sherehe hizo.

Sherehe za “Milango Wazi ya Misikiti” zilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1997 kutokana na kuongezeka kampeni za chuki dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani. Takwimu zinaonesha kuwa kuna zaidi ya Waislamu milioni nne (4,000,000) nchini Ujerumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!