Msikiti wa kihistoria wa Süleymaniye  mjini Istanbul Uturuki ni turathi ya kihistoria ya kipindi cha utawala wa Uthmania (Ottoman Empire) na licha ya kupita zaidi ya karne nne na nusu yaani miaka 463, lakini bado umejibakishia hadhi, heshima na mvuto wa hali ya juu. Msikiti Süleymaniye ni katika majengo yanayoongeza mvuto wa mji wa Istanbul.

Msikiti huo ulijengwa kwa amri ya Sultan Suleiman I, ambaye alikuwa mfalme wa 10 wa Uthmania. Muhandisi wa msikiti huo na majengo ya pembeni mwake alijulikana kwa jina la Mimar Sinan na ujenzi wake ulimalizika tarehe 15 Oktoba 1557 Milaadia. Kama tulivyosema, Msikiti Süleymaniye ni katika nembo za kihistoria za mji wa Istanbul na ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Wataalamu wengi wanasema kuwa, msikiti huo ndiyo turathi muhimu zaidi ya kihistoria iliyoachwa na silisila ya wafalme wa Uthmania. Ujenzi wa msikiti huo pamoja na skuli na maktaba zake kadhaa pembeni mwake ulianza mwaka 1550 Milaadia na ulimalizimika baada ya kupita miaka saba ya kazi nzito na isiyosita.

Mmoja wa wanahistoria aliyejikita katika historia ya utawala wa Uthmania anayejulikana kwa jina la Ibrahim anasema, takriba kilo 3,200 za dhahabu ziligharamia ujenzi wa msikiti huo na majengo yake mengine. Zaidi ya wafanyakazi 3,000 walishiriki kwenye ujenzi wa Msikiti wa Süleymaniye.

Anasema, wakati wa baridi kali, wafanyakazi wapatao 2,000 walikuwa wanafanya kazi kwa wakati mmoja ili ujenzi wa msikiti huo wa kihistoria usisite na umalizike katika muda uliopangwa.

Hatimaye baada ya kupita miaka saba, ujenzi wa Msikiti wa Süleymaniye na majengo ya pembeni mwake ulikamilika mjini Istanbul. Msikiti huo ulifunguliwa siku ya Ijumaa ya tarehe 15 Oktoba, 1557 Milaadia iliyosadifiana na sherehe za skukuu ya Mfunguo Tatu yaani mwezi 11 Dhulhija mwaka 964 Hijria. Sherehe za ufunguzi wa Msikiti huo zilihudhuriwa na Sultan Suleiman wa Kwanza mwenyewe na viongozi wa ngazi za juu wa serikali yake. Msikiti huo ulifunguliwa kwa ufunguo ambao Sultan Suleiman I alimpa mhandishi wa majengo hayo ya kihistoria, Mimar Sinan. Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za Msikiti wa Süleymaniye.

(Visited 101 times, 2 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!